Mtangazaji
wa kipindi cha njia panda Dr Isac ameonekana kusikitishwa na kumlilia
mtayarishaji wa kipindi hicho Jacky, "Jacky Njiapanda" ambae ameuwawa
kikatili na watu wasiojulikana jumamosi ya wiki iliyopita
Ilikua
ni miaka kumi iliyopita (10) mwaka 2004, nikiwa ndio kwanza nimean
za kufanya kazi chini ya kaka yangu Dr Sebastian Ndege na chini ya
uangalizi wa karibu sana wa boss Ruge Mutahaba na Boss Joseph Kussaga
nilipokutana na wewe mdogo wangu Jackline Masanja kupitia Njiapanda
ulipokuwa unatafuta msaada ukiwa mgonjwa sana.
Nakumbuka Dr Sebastian Ndege alipokuona tu alikubaliana na mimi kuwa tuache kila
mpango tuliokua nao tuweke nguvu zote kwako. Kweli ulikua unaonekana
ni mgonjwa, Kwa kutumia nafasi ya Dr Ndege kipindi hiko akiwa ndio
anakaribia kumaliza masomo yake ya udaktari na mimi ndio kwanza nikiwa
mwaka wa pili wa udaktari tulifanikiwa ku hakikisha kuwa unapata
matibabu ya haraka uliyokua unayahitaji sana.
Ulikua
shujaa sana kukubali kusema kuwa uko tayari Dr Ndege atangaze hali
yako mbele ya uma wa WaTanzania na kwa ruhusa yako tukafanya kipindi na
wewe huku ukiwa mgonjwa na ukasema kuwa umeathirika na kwa kipindi
kile kinga yako ilikua chini sana (CD4 zilikua 4).
Wewe
ulikua ni watu wa mwanzo kabisa kuja mbele ya umma kuongea kuhusu hali
halisi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na maradhi ya UKIMWI.
Tulikuita shujaa na Muhimbili ulipokua unatibiwa kipindi kile wahudumu
wote walikuita Jackie wa Njiapanda (ndio chanzo cha kumuita jina hilo
miaka yote hii). Kutokana na juhudi nyingi zilizofanyika ulipona kabisa
na ukarudi kwenye hali yako ya kawaida ya kawaida na ukaendelea na
maisha yako.
Kutokana na yote yaliyotokea mimi na Dr Ndege tukaona ni vyema kama tutakuomba ukae na sisi kama Njiapanda na uendelee kutusaidia kwa kuwa Nji apanda ilikua imekua sana na waliokua wanahitaji msaada walikuwa wanaongezeka kila kukicha. Hukusita kukubali na kuanzia miaka hiyo ukawa unatusaidia kushughulika na wote wanaohitaji msaada wa Njiapanda. Ni wengi uliwachukua na kukaa nao kwako ingawa hali yako ya kiuchumi haikua nzuri sana kusema eti wewe ni tajiri.
Miaka ilienda na ukaendelea kupambana na maisha huku ukiendelea vyema. Nakumbuka vizuri sana sakata la dawa ya Babu wa Loliondo lilipoanza mimi na wewe tulikua hasi na chanya. Mimi nilikua napinga sana kwa kuwa nilikua na sababu za kisayansi na wewe siku zote ulikua unakasirika kwa kuwa ulikua ukiamini kuwa dawa inaponya. Ukaniomba nikuruhusu uende na kweli tukakubaliana tukafanya mchakato na ukaenda. Tukakubaliana kuwa mimi nachohitaji ni kimoja tu nacho ni kukutumia wewe kama somo kwa hiyo tukarekodi kila kitu kabla hujaenda kwa babu na tukafanya kipindi maalum.
Ukasema
kinga yako ni ngapi na kila kitu wala hukuogopa. Ukaenda Loliondo
ukanyweshwa kikombe na ukarudi. Tukafanya kipindi ukasema unaendelea
viz uri. Tukaendelea na vipimo na maisha yakaenda. Miezi miwili
baadae nakumbuka nilikua nimekaa kliniki nikakuona kwa chini unatembea
huku unajikongoja, nikakufuata pamoja na manesi wa pale clinic
tukakuchukua tukaendelea na uchunguzi tukagundua kuwa kinga yako
imeshuka sana kwa kuwa baada ya kwenda kwa babu hukuendelea na dawa
(kinga ilikua 14).
Tukaanza
kufanya jitihada za kuhakikisha afya yako inarudi kuwa nzuri na kweli
ukawa Ok na tukafanya kipindi tena kuhusu kilichotokea. Kama kawaida
ukawa shujaa na kusema kila kitu. Kupitia kwako waTanzania wakajifunza
mengi kuhusu ki kombe cha babu na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa
ujumla. Kupitia wewe Jackline Masanja watu wakafanya maamuzi huku
wanajua, ambayo kisayansi ni jambo la maana sana. Jackie mdogo wangu,
mimi na Dr Sebastian Ndege kamwe tusingeweza kuifikisha Njiapanda
ilipofika bila ya ushujaa wako, bila ya utayari wako wala bila ya uwazi
wako.
Sio
tu kwa kupitia story yako watu wamejifunza mengi kuhusu maambukizi ya
virusi vya UKIMWI bali pia mchango wako wa kusaidia Njiapanda na watu
wa njiapanda tumeweza kufanya mengi sana. Nakumbuka habari ya wamasai
uliileta wewe, habari ya yule m sichana aliyelazimishwa kufanya
mapenzi na mbwa ilitoka kwako, watoto wa mitaani wanaolazimishwa
kufanya mapenzi kinyume cha maumbile pale kariakoo uliifuatilia wewe
mpaka ukalala kariakoo usiku kucha kuifuatilia. Ni nyingi sana Jackie.
Jackie,
kwangu mimi na kwa Dr Sebastian Ndege wewe ni mdogo wetu yule yule wa
miaka 10 iliyopita. Ulikua unatuita kaka na sisi tukauita mdogo wetu.
Nakumbuka hata mambo yalipokua magumu nikgombana na ma boss wangu kina
Ruge nilikua nakuomba ukaniombee msamaha maana boss Ruge alikua
anakupenda sana kama mdogo wake, nilijua kuwa ukisema tu boss
atanisamehe hahahaaaaa…asante sana mdogo wangu kwa kuokoa jahazi mara
kwa mara lol.
Leo
hii nimeamua kuandika huu waraka mrefu kwako wewe Jackie kwa kupitia
ndugu zangu wa Facebook na platforms nyingine kwa sababu, siku ya
jumamosi 22 November 2014 nilipata ujumbe kutoka kwa rafiki yangu na
mfanyakazi mwenzangu Geah Habibu kukuhusu wewe mdogo wangu, kwamba
mwili wako umekutwa ukiwa umekwishafariki.
Sio
tu kuwa kifo chako kilikua cha kawaida bali inaonekana umeuawa. Kwa
bahati mbaya sana kw a sasa siko nchini kwa hiyo sikuamini na
sikuweza kufanya chochote mpaka pale nilipoona picha yako. Kusema
ukweli bado sikuamini so nikaongea na Douglas na Amani (watengenezaji
wa Njiapanda) wafuatilie hii habari. Mwisho wa siku ni kweli ikaonekana
kuwa umeuawa tena kikatili.
Nikawasiliana
na kaka yangu Dr Sebastian Ndege naye hakuamini. Jumapili ilipofika
nikasema nisiseme chochote maana naona bado si kweli (nisamehe mdogo
wangu) nikajikaza nikafanya Njiapanda bila kusema chochote. Jana
jumatatu ndio Geah akanihakikishia kuwa ni kweli umefariki na baba yako
amekutambua na msiba kweli uko.
Nimelia
sana, sijui kwa nini umefanyiwa ukatili huu, siwezi kusema chochote
kwa kuwa sijui, lakini kitu kimoja nachoamini na kinachoniuma moyoni
mwangu ni kuwa mimi, wewe na Seba tumepambana sana Zaidi ya miaka kumi
kuhakikisha unakua ok na afya njema, najiuliza swali yote hiyo ilikua
kwa nini? JE NI KWELI KUWA JUHUDI ZOTE HIZO ZILIKUA KUKUTAYARISHA UJE
UUWAWE KINYAMA NAMNA HII??
Mwenyezi
Mungu pekee ndie anayejua kilichotokea na ndiye anayejua hukumu ya
kila mmoja wetu. Jack ie mdogo wangu umeenda, umeacha wadogo zako na
familia yako. Mungu akulaze mahali pema peponi mdogo wangu, naamini
sasa utapumzika maana umehangaika sana na haya maisha.
Familia
yako naamini Mungu atabariki itakaa salama na yote yatakua heri. Dr
Ally Kaduma na clinic nzima ya IDC wanakulilia, Clinic ya watoto na ya
watu wazima ya DarDar wanakulilia watamiss unga wako ule wa uji wa
watoto uliokua unaleta.
Clouds
Media yooote inakulilia, boss Ruge anakulilia, familia yote ya
Njiapanda inakulilia , kina mama Derick na kina brother Gelvas na kaka
yako mkubwa kabisa Danny Kiondo wanakulilia.
Mimi,
Dr Ndege, Mishy Singano, Jackie Chengula (tunamwita JACKIE mkubwa kwa
kuwa wewe ulikua unajiita Jackie mdogo), Simon Simalenga, Amani Siri,
Douglas Pius, Arnold Kayanda (hadi harusi yake ulisimamia), Geah Habib,
Regina Mwalekwa, Ruge Mutahaba, Team Njiapanda ya tangu 2003 mpaka ya
leo wote tunakulilia mdogo wetu.
Kwetu
sisi wote wewe bado ni Jackie wa Njiapanda yule wa tangu 2004. Mdogo
wetu mwenye upendo na uliyekua tayari kutumia hadithi ya maisha yako
kama fundisho kwa wengine. Wewe ni shujaa na kamwe hilo halitokaa
libadilike. Sheria itachukua mkondo wake kwa wote waliosababisha kifo
chako na Mungu atamhukumu kila mtu kwa jinsi alivyotenda.
Ninalia
sana, ninahuzunika sana ninatamani ningeweza kufanya lolote lakini
nimeshindwa ndio maana nikashindwa kukuokoa na hili, Mungu atanisamehe
maisha yameniweka mbali na wewe mdogo wangu mpaka mauti yamekukuta.
Kibaya Zaidi ni kuwa hata kukuzika sitaweza kwa kuwa niko mbali na
nyumbani. Lakini ninaamini huko ulipo utafu rahi kufahamu kuwa
ninafanya yote haya ninayofanya ili niweze kuwasaidia waTanzania
wenzetu vizuri Zaidi nao wawe na afya njema kama nilivyojitahidi
kufanya yako iwe.
Ulale pema peponi mdogo wangu, Jackline Masanja..
Mungu ibariki familia yako,
Mungu ibariki Clouds Media Group
Mungu ibariki Njiapanda
Post a Comment