Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Rajabu
Rutengwe kuomboleza vifo vya watu 11 ambapo wengine kadhaa walijeruhiwa
katika ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 27 Novemba, 2014.
Ajali hiyo
ilitokea katika eneo la Mkanyageni Mkoani Tanga baada ya basi dogo aina
ya Toyota Coaster Na. T 410 BJD iliyokuwa ikitoka Tanga Mjini kuelekea
Lushoto kugongana na Lori aina ya Scania Na. T 605 ABJO.
“Nimepokea
kwa masikitiko makubwa taarifa ya kupotea ghafla kwa maisha ya watu 11
na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea
katika Mkoa wako wa Tanga”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake na kuongeza:
“Naomba
upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana
na vifo hivyo, na kupitia kwako, naomba salamu za pole ziwafikie watu
wote waliopotelewa na ndugu na jamaa zao kwenye ajali hiyo”.
Rais
Kikwete amesema anawaomba wote waliopoteza ndugu na jamaa zao kwenye
ajali hiyo wawe watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha
maombolezo, na amewahakikishia kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote
cha maombolezo.
“Kwa
wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo, namwomba Mungu awajalie ahueni na
wapone haraka, ili warejee tena katika hali zao za kawaida. Namwomba
Mola azipokee na kuzilaza mahala pema peponi Roho za Marehemu wote,
Amina”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
27 Novemba, 2014
Post a Comment