Kocha wa Prisons, David Mwamaja ana mwonekano tofauti na makocha wengine wa Ligi Kuu Bara kutokana na mwili mkubwa alionao.
Hata hivyo, Mwamaja anasema ana maumivu ya goti ambayo yanamnyima furaha na amekuwa akiishi na maumivu hayo kwa miaka 34.
“Mwaka 1980 nilikuwa namba nane wa Kurugenzi
Arusha, tulicheza mechi na Morani ya Arusha, nikiwa naambaa na mpira
kwenda kufunga mchezaji wa Morani anaitwa King’ang’a alinichezea rafu
mbaya.
“Nilipata maumivu makali ya goti ingawa kwa miaka
ile sikupata matibabu ya maana, na ndiyo ukawa mwisho wangu wa kucheza
soka, ila rafiki yangu mmoja alinishauri niingie kwenye ukocha na mimi
nikakubali,” anasema Mwamaja.
Alipoambiwa goti lake limesagika
“Licha ya kuingia kwenye ukocha bado sikuwa na
furaha kutokana na maumivu niliyokuwa nayapata kwani kuna wakati goti
linaniuma hata wiki nzima mfululizo na inapotokea natumia dawa za
maumivu linatulia, lakini baada ya muda linaanza tena kuuma”.
Aliongeza; “Mwaka jana nilienda kupima majibu
niliyopata yanilisikitisha kwani niliambiwa goti langu la kushoto
limesagika hivyo tiba pekee ni kwenda India kufanyiwa operesheni na
kuwekewa kifaa bandia kitakachonisaida kupunguza maumivu ninayopata,
hata hivyo nilishindwa kwenda India kwa sababu nilikosa fedha,” anasema
Mwamaja.
Anasema tatizo hilo halitokani na uzito mkubwa kilo 110 alizonazo.
Mali kauli ilivyomtibulia usajili wa Ngassa
“Nikiwa kocha wa Ruvu Shooting kipindi tupo Daraja
la Kwanza tulicheza mechi yetu ya mwisho Shinyanga, mechi ambayo
ilitupandisha kucheza Ligi Kuu, huko ndipo nilimuona Mrisho Ngassa na
Mwinyi Kazimoto ambao walikuwa wakichezea timu pinzani,” anasema
Mwamaja.
Anasema alivutiwa na uchezaji na umri wao mdogo hivyo kupendekeza wasajiliwe kwenye kikosi chake.
“Kwa Ngassa tuligonga mwamba kwa kuwa tuliingia na
kigezo kwamba atapata ajira ila yeye alitaka fedha ambazo hatukuwa nazo
huku Kazimoto akikubali kuajiriwa hivyo tukamsajili,” anasema Mwamaja
baba wa watoto watano.
Post a Comment