Utafika wakati lazima ufanye uamuzi mgumu


Watafiti wa maisha ya binadamu na tabia zake, wanaamini kuwa kila mmoja utafika wakati atakutana na jambo litakalomlazimu kufanya au kutoa uamuzi mgumu.
Bila kujali jambo gani, lini na aina ya uamuzi anaoweza kuutoa, lakini ukweli unabaki palepale kwamba ipo siku lazima binadamu ataingia kwenye hali hiyo.
Katika maisha ya sasa yaliyojaa kila aina ya changamoto, chuki, visasi, migogoro na mabadiliko yenye ulazima ili kwenda sambamba na mahitaji ya maisha, yanawalazimu watu kufanya mambo ambayo hawatarajii.
Hata hivyo, kuna tofauti. Wapo ambao kutoa kwao uamuzi mgumu hutokana na shinikizo, hoja na mitazamo kutoka nje, wengine hufanya hivyo bila kusubiri misukumo ya nje bali ni kutokana na msuto wa dhamira kutoka ndani ya moyo.
Hongera kwa aliyekuwa kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi kwa kuchukua hatua ya kufanya uamuzi mgumu wa kuachana na timu hiyo bila shinikizo. Ni kama nilivyosema awali, Mwambusi amekutana na wakati ambao umemlazimu kufanya uamuzi mgumu ili kulinda heshima yake. Hakuna anayependa kuharibu ajira yake, lakini una sababu gani ya kusubiri kama mambo yameshaharibika?
Alichofanya Mwambusi ni ujasiri mkubwa kwa sababu, baadhi yetu wakati mwingine, iwe kwa kulewa madaraka au kwa lengo la kujishibisha, tunashindwa kutoa uamuzi mgumu hadi tulazimishwe.
Inawezekana kabisa Mwambusi amebeba msalaba ambao wengi waliutarajia. Kikosi chake kililewa sifa baada ya kufanya vizuri msimu uliopita kiasi cha kushika nafasi ya tatu ligi ilipomalizika.
Ilishangaza kwa timu ngeni, isiyo na wachezaji wenye majina na kocha wa ‘kawaida’ kupata matokeo mazuri kuizidi hata klabu kongwe ya Simba iliyojaza nyota kibao wa ndani na nje.
Kilichoiponza City ni kulewa mafanikio ya msimu uliopita na kudhani kuwa, wanaweza kufanya hivyo kirahisi msimu uliofuata. Walikosea!
Walidhani ligi ni peke yao, kwamba timu zingine zilizofanya vibaya msimu ambao wao walifanya vizuri, basi zingebaki kwenye nafasi hiyo ya kufanya vibaya. Walijidanganya!
Kila mmoja, kwa maana ya mashabiki wa soka Mbeya walikuwa wakisifu mafanikio ya timu hiyo, lakini, ni kwa kiasi gani walikuwa bega kwa bega kuisaidia kufanya vizuri msimu huu?
Sasa Mwambusi amefanya uamuzi mgumu, amejiuzulu. Ameiacha timu kwenye wakati mgumu.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post