Watafiti wa maisha ya binadamu na tabia zake, wanaamini kuwa
kila mmoja utafika wakati atakutana na jambo litakalomlazimu kufanya au
kutoa uamuzi mgumu.
Bila kujali jambo gani, lini na aina ya uamuzi
anaoweza kuutoa, lakini ukweli unabaki palepale kwamba ipo siku lazima
binadamu ataingia kwenye hali hiyo.
Katika maisha ya sasa yaliyojaa kila aina ya
changamoto, chuki, visasi, migogoro na mabadiliko yenye ulazima ili
kwenda sambamba na mahitaji ya maisha, yanawalazimu watu kufanya mambo
ambayo hawatarajii.
Hata hivyo, kuna tofauti. Wapo ambao kutoa kwao
uamuzi mgumu hutokana na shinikizo, hoja na mitazamo kutoka nje, wengine
hufanya hivyo bila kusubiri misukumo ya nje bali ni kutokana na msuto
wa dhamira kutoka ndani ya moyo.
Hongera kwa aliyekuwa kocha wa Mbeya City, Juma
Mwambusi kwa kuchukua hatua ya kufanya uamuzi mgumu wa kuachana na timu
hiyo bila shinikizo. Ni kama nilivyosema awali, Mwambusi amekutana na
wakati ambao umemlazimu kufanya uamuzi mgumu ili kulinda heshima yake.
Hakuna anayependa kuharibu ajira yake, lakini una sababu gani ya
kusubiri kama mambo yameshaharibika?
Alichofanya Mwambusi ni ujasiri mkubwa kwa sababu,
baadhi yetu wakati mwingine, iwe kwa kulewa madaraka au kwa lengo la
kujishibisha, tunashindwa kutoa uamuzi mgumu hadi tulazimishwe.
Inawezekana kabisa Mwambusi amebeba msalaba ambao
wengi waliutarajia. Kikosi chake kililewa sifa baada ya kufanya vizuri
msimu uliopita kiasi cha kushika nafasi ya tatu ligi ilipomalizika.
Ilishangaza kwa timu ngeni, isiyo na wachezaji
wenye majina na kocha wa ‘kawaida’ kupata matokeo mazuri kuizidi hata
klabu kongwe ya Simba iliyojaza nyota kibao wa ndani na nje.
Kilichoiponza City ni kulewa mafanikio ya msimu
uliopita na kudhani kuwa, wanaweza kufanya hivyo kirahisi msimu
uliofuata. Walikosea!
Walidhani ligi ni peke yao, kwamba timu zingine
zilizofanya vibaya msimu ambao wao walifanya vizuri, basi zingebaki
kwenye nafasi hiyo ya kufanya vibaya. Walijidanganya!
Kila mmoja, kwa maana ya mashabiki wa soka Mbeya
walikuwa wakisifu mafanikio ya timu hiyo, lakini, ni kwa kiasi gani
walikuwa bega kwa bega kuisaidia kufanya vizuri msimu huu?
Sasa Mwambusi amefanya uamuzi mgumu, amejiuzulu. Ameiacha timu kwenye wakati mgumu.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق