MWANAFUNZI mmoja wa sekondari ya Hunyari, Wilaya hapa, Mkoa wa Mara,
amehukumiwa kwenda jela miaka 30 na kuchapwa viboko 12 na Mahakama ya
Wilaya hiyo kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa shule ya msingi (18) jina
linahifadhiwa.
Akimsomea shitaka lake, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
hiyo, Safina Simufukwe, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Masoad Mohamed,
alisema mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 24 aliyekuwa anasoma kidato
cha nne katika shule hiyo alitenda kosa hilo mnamo Novemba 17, mwaka
huu majira ya saa 4:00 usiku katika kijiji cha Sarawe.
Mohamed alisema mshitakiwa ni mwanafunzi anayesubiri matokeo ya
kidato cha nne baada ya kufanya mtihani mwaka huu, alimbaka mwanafunzi
huyo anayesoma darasa la saba katika shule ya msingi Sarawe, baada ya
kumfungia ndani ya chumba chake nyumbani kwao kwa muda wa siku mbili
mfululizo.
Alisema kabla ya mwanafunzi huyo kukamatwa, viongozi wa kijiji hicho
walipata taarifa ya mwanafunzi huyo kumfungia ndani mwanafunzi mwenzake
na kumbaka kwa siku hizo.
Aliongeza kuwa viongozi wa kijiji hicho wakiwa na wananchi walikwenda
katika eneo la tukio majira ya usiku na kumkuta mwanafunzi huyo
akimfanyia kitendo hicho mwenzake na ndipo alikamatwa na kupelekwa
katika kituo cha polisi Nyamuswa.
Baada ya kusomewa shitaka lake mwanafunzi huyo alikiri kufanya kosa
hilo, huku akidai kuwa mwanafunzi huyo wa darasa la saba ni mpenzi wake
wa siku nyingi na kwamba anaomba asamehewe na Mahakama hiyo.
Kutokana na kukiri kosa hilo Hakimu Simufukwe alimtia hatiani na
kumuhuku kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kuchapwa viboko 12, ili
liwe fundisho kwake na kwa wanafunzi wengine, pamoja na watu wenye
wenye tabia au nia ya kutenda kosa ya ubakaji.
إرسال تعليق