Nchi yatikiswa

Dodoma. Hatimaye mtikisiko wa tano umetimia na nchi kutikiswa; ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) imependekeza kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Nishati na Madini, naibu wake na katibu mkuu wa wizara hiyo wawajibishwe kutokana na kuhusika kwao kwenye sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kutunza fedha za gharama za uwekezaji (capacity charge) baada ya kuibuka mzozo wa kimkataba baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni binafsi ya IPTL ambayo iliingia mkataba wa kufua umeme na kuliuzia nishati hiyo shirika hilo la umma.
Ripoti hiyo ilisomwa jana bungeni kwa kupokezana kati ya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe na Makamu mwenyekiti, Deo Filikunjombe baada ya majadiliano marefu kwenye vikao vya ndani vya CCM na Kamati ya Uongozi wa Bunge na jitihada kubwa za kutaka isisomwe na kujadiliwa.
Ripoti hiyo ilitokana na ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilianika ukiukwaji mkubwa wa taratibu wakati wa uchotaji wa fedha hizo pia mahojiano na mkurugenzi mkuu wa Takukuru na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Waziri Pinda ametiwa hatiani na kamati hiyo kutokana na kujua kuwapo kwa ufisadi huo na kauli zake kuwa fedha hizo hazikuwa mali ya umma, wakati Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema ameonekana kutoishauri vizuri Serikali na pia kuagiza fedha hizo zitolewe kwenye akaunti hiyo, wakati Waziri Sospeter Muhongo hakuchukua hatua wakati akijua kuwapo kwa sakata hilo, huku naibu wake, Stephen Masele akitiwa hatiani kwa kulidanganya Bunge.
Kamati pia imependekeza uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi utenguliwe kutokana na kuingia makubaliano ya kutoa fedha bila ya kujiridhisha kikamilifu kuhusu uamuzi wa hukumu ya mahakama ya Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Kiuwekezaji (ICSID).
Iwapo mjadala huo, unaotazamiwa kuendelea leo, utaafiki hatua hizo zichukuliwe, Rais atalazimika kuunda Serikali upya kwa mara ya pili tangu alipofanya hivyo mwaka 2008 wakati wa sakata la Richmond, ambalo lilihusu umeme. Pia atakuwa akifanya mabadiliko ya mawaziri kwa mara ya tano kutokana na wasaidizi hao kujikuta kwenye kashfa.
Kuhusu Pinda
Akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Filikunjombe alisema katika suala hilo, Pinda anahusika kwa kuwa katika Katiba Ibara ya 52(1) inaeleza kuwa waziri mkuu atakuwa na madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Pia ibara ya 52(2) inasema waziri mkuu atakuwa kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni. Kutokana na ibara hizo, Filikunjombe alisema baada ya kupitia vielelezo vilivyomo kwenye ripoti ya CAG, kamati imejiridhisha pasipo shaka kwamba Waziri Mkuu alikuwa ana taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa kuchotwa fedha katika Akaunti ya Escrow.
“Ushahidi uliotolewa na CAG kwenye kamati unaonyesha kuwa waziri mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hili na kamati imesikitishwa kuona kuwa Waziri Mkuu hakuchukua hatua zozote kuzuia muamala huu usifanyike,” alisema Filikunjombe
- Soma Hapa Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post