Dodoma. Hatimaye mtikisiko wa tano umetimia na nchi kutikiswa;
ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) imependekeza kuwa Waziri
Mkuu Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Nishati na Madini, naibu
wake na katibu mkuu wa wizara hiyo wawajibishwe kutokana na kuhusika
kwao kwenye sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka kwenye Akaunti
ya Tegeta Escrow.
Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kutunza
fedha za gharama za uwekezaji (capacity charge) baada ya kuibuka mzozo
wa kimkataba baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni
binafsi ya IPTL ambayo iliingia mkataba wa kufua umeme na kuliuzia
nishati hiyo shirika hilo la umma.
Ripoti hiyo ilisomwa jana bungeni kwa kupokezana
kati ya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe na Makamu mwenyekiti, Deo
Filikunjombe baada ya majadiliano marefu kwenye vikao vya ndani vya CCM
na Kamati ya Uongozi wa Bunge na jitihada kubwa za kutaka isisomwe na
kujadiliwa.
Ripoti hiyo ilitokana na ukaguzi uliofanywa na
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilianika
ukiukwaji mkubwa wa taratibu wakati wa uchotaji wa fedha hizo pia
mahojiano na mkurugenzi mkuu wa Takukuru na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA).
Waziri Pinda ametiwa hatiani na kamati hiyo
kutokana na kujua kuwapo kwa ufisadi huo na kauli zake kuwa fedha hizo
hazikuwa mali ya umma, wakati Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema
ameonekana kutoishauri vizuri Serikali na pia kuagiza fedha hizo
zitolewe kwenye akaunti hiyo, wakati Waziri Sospeter Muhongo hakuchukua
hatua wakati akijua kuwapo kwa sakata hilo, huku naibu wake, Stephen
Masele akitiwa hatiani kwa kulidanganya Bunge.
Kamati pia imependekeza uteuzi wa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi utenguliwe kutokana na
kuingia makubaliano ya kutoa fedha bila ya kujiridhisha kikamilifu
kuhusu uamuzi wa hukumu ya mahakama ya Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi
wa Migogoro ya Kiuwekezaji (ICSID).
Iwapo mjadala huo, unaotazamiwa kuendelea leo,
utaafiki hatua hizo zichukuliwe, Rais atalazimika kuunda Serikali upya
kwa mara ya pili tangu alipofanya hivyo mwaka 2008 wakati wa sakata la
Richmond, ambalo lilihusu umeme. Pia atakuwa akifanya mabadiliko ya
mawaziri kwa mara ya tano kutokana na wasaidizi hao kujikuta kwenye
kashfa.
Kuhusu Pinda
Akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo, Makamu
Mwenyekiti wa PAC, Filikunjombe alisema katika suala hilo, Pinda
anahusika kwa kuwa katika Katiba Ibara ya 52(1) inaeleza kuwa waziri
mkuu atakuwa na madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa
siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Pia ibara ya 52(2) inasema waziri mkuu atakuwa
kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni. Kutokana na ibara hizo,
Filikunjombe alisema baada ya kupitia vielelezo vilivyomo kwenye ripoti
ya CAG, kamati imejiridhisha pasipo shaka kwamba Waziri Mkuu alikuwa ana
taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa kuchotwa fedha katika
Akaunti ya Escrow.
“Ushahidi uliotolewa na CAG kwenye kamati
unaonyesha kuwa waziri mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hili na
kamati imesikitishwa kuona kuwa Waziri Mkuu hakuchukua hatua zozote
kuzuia muamala huu usifanyike,” alisema Filikunjombe
- Soma Hapa Mwananchi
- Soma Hapa Mwananchi
إرسال تعليق