Taarifa kwamba nchi za Kenya na India zimeipita kwa mbali Tanzania kwa kusafirisha madini ya Tanzanite yanayopatikana hapa nchini pekee na kuyauza katika soko la dunia ni jambo ambalo siyo rahisi kuliamini.
Nasema siyo rahisi kuamini kwa sababu haingii
akilini hata kidogo, mtu ambaye halimi mahindi anaibuka kinara wa kuuza
sokoni mahindi yako anayoyaiba shambani kwako.
Ni heri kama angekuwa anakuja kununua kwa njia ya kawaida na wewe ukanufaika.
Nilimsoma kwa makini Kamishna wa Madini katika
Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja hivi karibuni kupitia
baadhi ya magazeti nchini akisema kwamba kwa mwaka jana, Tanzania
haikufikia hata nusu ya Kenya kwa mauzo ya madini hayo ya vito.
Mwaka jana pekee, Kenya ilisafirisha na kuuza nje
ya nchi Tanzanite yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 100 milioni
(Sh173 bilioni), dhidi ya Dola 38 milioni (Sh45.5 bilioni), zilizouzwa
na Tanzania.
Katika kipindi hicho cha mwaka jana, India iliuza
Tanzanite zenye thamani ya zaidi ya Dola 300 milioni za Marekani(Sh509
bilioni) kiasi cha baadhi ya wanunuzi wakubwa, hasa kutoka Marekani
kujiuliza iwapo madini hayo yanachimbwa India.
Mmoja wa wanunuzi wakubwa wa madini ya vito kutoka
Marekani, aliwahi kuwauliza viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini
iwapo kuna migodi ya Tanzanite India kwa sababu akifika huko hupata
Tanzanite bora na zenye ukubwa kuliko anayopata Tanzania.
Taarifa zinaeleza kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya
Tanzanite inayopatikana Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara,
huuzwa kwa njia za panya nje ya nchi na kwamba Serikali imeanza kuchukua
hatua.
Kama nilivyosema awali, hili ni jambo la
kushangaza sana. Ninajiuliza; hivi haya madini nani anayeyatorosha
kwenda nchi za nje? Ni wazi kuwa watu wachache waliopewa jukumu la
kusimamia sekta ya madini, wamekuwa wakishirikiana na watu wa nje
kutorosha madini hayo.
Tumejua wizi wa madini haya kwa sababu tu
yanapatikana pekee Tanzania. Tujiulize wizi huu wa madini yetu ukoje
katika madini mengine ambayo pia yanapatikana katika nchi nyingine?
Kwa hakika, raslimali za nchi hii zinaliwa na watu wengine, huku Watanzania wakibaki mikono mitupu.
Ni wazi kuwa watu wanaotorosha madini haya
hawapiti vikachani, wanapita katika maeneo ya mipaka yetu, lakini ulafi
wa baadhi ya maofisa wa Serikali ndiyo imetufikisha tulipo kwa sasa
إرسال تعليق