
Rais Kikwete alisema binafsi hakutaka kufanya
ugonjwa wake siri, lakini alishauriwa kutotangaza ugonjwa huo ili
asiwatie wananchi hofu. Kwa sasa hali ya afya yake ni nzuri.
Kuhusu sakata la escrow, Rais Kikwete alisema
hawezi kuyasemea kwa vile hana taarifa za kutosha kuhusu yanayoendelea
Dodoma na kwamba pindi atakapopata yanayojiri huko ataweza kuyasema kama
ataona kuwa kuna haja ya kuyasema.
Rais Kikwete ambaye hakuwepo nchini kwa takriban
siku 20 akiwa kwenye matatibabu, alisema kuwa Septemba 27, 2013
alibainika kuwa na ugonjwa wa saratani ya tezi dume, lakini alikaa nayo
kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kufanyiwa upasuaji kutokana na shughuli
nyingi za kikazi.
“Uchunguzi wa kipimo cha PSA (Prostate-Specific
Antigen) ulibaini nina tatizo la tezi dume ambalo lilizidi kiwango
kinachotakiwa mwilini. PSA yangu kwa zaidi ya miaka mitatu ilikuwa
inapanda kwa kiwango kikubwa hali iliyoashiria kuwa kuna tatizo ambalo
linahitaji matibabu,” alisema.
Alisema madaktari walimshauri kufanya upasuaji
lakini alilazimika kuomba kufanyiwa Julai 2014, ili kupata muda wa
kupokea Rasimu ya Katiba. Hata hivyo, kwa vile Bunge la Katiba
halikuisha kama ilivyotarajiwa na kwamba hadi Julai Bunge lilikuwa
halijamaliza kazi yake, aliomba kufanyiwa Novemba 2014.
Rais Kikwete alisema madaktari walimshauri kuwa
asikose kufanyiwa mwezi huo kwa vile akichelewa sana saratani inaweza
kusambaa hadi viungo vingine vya mwili.
Alisema kuwa kufanikiwa kufanyika kwa upasuaji
kumempa nafuu sana na kumeshusha mizigo miwili aliyokuwa anayo. Alisema
kuwa hofu ya kwanza aliyokuwa nayo ni baada ya kuambiwa kuwa ana
saratani. Hivyo alikuwa ana hofu kwamba ugonjwa huo ungeweza kuenea
sehemu nyingine mwilini.
Rais Kikwete alisema mzigo wa pili ni kutokana na
jambo hilo kukaa nalo peke yake kwa muda mrefu. Alisema kuwa alimwambia
mkewe baada ya miezi minane na kumtaka asimwambie mtu hadi atakaposema
mwenyewe.
Hivyo kitendo cha kukaa na ugonjwa huo bila ya
kumwambia mtu ulikuwa ni mzigo mkubwa na kwamba hata mkewe aliweza
kutunza siri ya ugonjwa wake mpaka siku nne kabla ya kwenda kufanyiwa
upasuaji.
Alisema kuwa aliliambia Baraza la Mawaziri kuhusu ugonjwa wake siku nne kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Pia, Rais Kikwete alisema anamshukuru Mungu kwa
kuwa madaktari katika Hospitali ya Johns Hospkings iliyoko Baltimore,
Jimbo la Maryland, Marekani wamethibitisha kuwa yu mzima, ingawa
atapaswa kupumzika kwa wiki nne kabla ya kuendelea na majukumu yake ya
kawaida.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment