Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la papo kwa hapo lililoulizwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, bungeni jana.
Mbowe katika swali lake alihoji kama haoni sababu ya kujiuzulu ili kupisha watu wengine wenye uwezo wamalizie ngwe iliyobaki ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne.
“Chini ya uongozi wako kama waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ukiwa kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, tumeiona serikali ikikumbana na matatizo na vikwazo vingi, ikiwamo operesheni tokomeza ambayo ilipelekea watu wengi kupoteza maisha," alisema Mbowe.
Aliongeza: "Wengine wakipata vilema, tumeona mauaji ya raia yakiendelea Kiteto hadi hatua ya sasa serikali bado haijaweza kuchukua hatua stahiki kukomesha mauaji hayo na bado yanaendelea.”
“Kumekuwa na migongano mbalimbali na kashfa mbalimbali kwa serikali, kashfa kubwa ambayo iko current sasa hivi, ikiwa ni pamoja na kauli zako ulizowahi kuzisema katika Bunge hili kwamba fedha zilizopotea za akaunti ya Escrow hazikuwa fedha za umma, zilikuwa za watu binafsi.”
“Je, waziri mkuu baada ya ripoti ya CAG kutolewa hadharani kuhusiana na fedha za Escrow na baada ya ripoti ya PCCB (Takukuru) kutolewa na hatimaye jana hapa bungeni kusomwa taarifa ya kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Serikali, nini msimamo wako kuhusu kauli yako ya awali kwamba fedha zile zilikuwa ni za watu binafsi na siyo fedha za umma.”
“Na ‘b'’ kwa uzito huo ukichanganya na matukio mengine mbalimbali ambayo yamepelekea fedheha kubwa kwa taifa letu, huoni kama ingekuwa mwafaka kwako binafsi na kwa taifa kupumzika kidogo ili kupisha nafasi kwa watu wengine kuweza kumalizia ngwe hii ya utawala wenu?,” alisema na kuhoji Mbowe.”
Kutokana na swali hilo la Mbowe, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema kwa kifupi “Huo unaitwa uchokozi,” alisema huku wabunge wakiangua vicheko.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema: “Mheshimiwa spika, inawezekana mheshimiwa Mbowe una shauku ya kutaka litokee hilo, lakini mambo haya yanategemea kama ndivyo Mungu kapanga au hapana.”
“Najua umeingiza mambo mengi sana kwenye jambo hili, lakini kubwa ni hilo ulilomaliza nalo. Ningeweza nikajaribu kujibu, lakini sina sababu ya kufanya hivyo. Sina sababu ya kufanya hivyo kwa sababu suala lenyewe ndiyo Subject (mada) ya mjadala hapa bungeni, ambao unaanza leo (jana),” alisema Pinda.
Pinda alisema ni vema suala hilo likasubiri mjadala utakapoanza kwa kuwa naye atapata nafasi ya kueleza kwa undani kuhusu suala hilo.
“Kwa hiyo, mimi nilikuwa nafikiri jambo la busara tusubiri mjadala utakavyokwenda naamini na mimi nitapata nafasi ya kusema mawili matatu.
“Kwa hiyo, nadhani mwisho wa yote nadhani Bunge litakuwa limefikia mahali ambapo tunaweza tukasema kwa uhakika ni hatua stahiki namna gani inaweza kuchukuliwa,”
alisema Pinda Hata hivyo, pamoja na Mbowe kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Waziri Mkuu na kumtaka kulijibu, hakulijibu, badala yake alinyamaza kimya.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment