Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mvomero,Iddi Abdallah.
Wanachama hao waliandamana kufuatia Kamati Kuu ya CCM Wilaya ya Mvomero kukata majina ya wagombea walioshinda na kurudisha majina ya walioshindwa ili wagombee nafasi za wenyeviti wa vijiji hivyo.
Mbali ya maandamano hayo, wanachama hao walifikia uamuzi wa kuhama chama hicho kutokana na Kamati Kuu ya CCM wilayani humo kubadilisha matokeo kwa kumpitisha Apronali Kahumba aliyeshindwa kwa kupata kura 308 na kumuondoa Juma Hassani aliyekuwa mshindi kwa kura 507.
Mwanachama wa CCM aliyejitambulisha kwa jina la Zuwena Rashidi alisema kitendo kilichofanywa na Kamati Kuu Wilaya kimewakatisha tama, huku akililaumu Jeshi la Polisi kwa kuzuia maandamano hayo akieleza ni kunyimwa uhuru.
Wananchi hao walirudisha kadi za CCM na kuamua kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wakizungumza kwa jazba, wanachama hao walisema wamechoka kuongozwa na watu wanaobebwa na chama badala yake wanahitaji viongozi waadilifu watakaosaidiana na wananchi kutatua kero mbalimbali za maendeleo katika kijiji cha Luhindo.
Wakati vurugu zikiendelea katika kijiji cha Luhindo, takribani wanachama 500 wamerudisha kadi za CCM na kumkabidhi Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mvomero, Kashikashi Saimanga, ambaye aliwapa kadi za Chadema.
Akizungumza na wananchi hao baada ya kupokea kadi zaidi 500, Saimanga alisema Chadema ni chama makini na kinasikiliza wananchi wake na kwamba maamuzi waliyochukua ya kuihama CCM ni sahihi kwani zama za kuburuzwa na kuchaguliwa viongozi zimepitwa na wakati na viongozi wanapimwa kwa utendaji wao.
Alisema Chadema itaendelea kusikiliza sauti za wananchi kwani serikali inajengwa kuanzia ngazi za chini na kuwataka wananchi wa Luhindo kutokata tamaa.
Akizungumza na wananchi hao akiwa kwenye gari la polisi, Diwani wa Kata ya Dakawa (CCM), Yusuph Athuman, alisema uamuzi uliotolewa na Kamati Kuu ya CCM wilayani humo ni wa mwisho na hauwezi kubadilishwa na kuwaeleza kuwa kama hawajaridhika wafanye wanachotaka.
Kiongozi huyo ambaye alizungumza kwa kejeli na jazba, alisema Kamati Kuu ya chama hicho haiendeshwi kwa kuburuzwa na wananchi na kuwa kamati ya siasa ya wilaya imeshapanga na hakuna kitakachobadilishwa.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mvomero, Iddi Abdallah, ambaye aliongoza askari wake kuzuia maandamnao hayo katikati ya barabara kuu ya Morogoro-Dodoma, alisema wananchi hawana haki ya kufanya maandamano bila kuwa na kibali cha polisi.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, Katibu wa CCM Wilaya ya Mvomero, Hamisi Kimati, alisema hana mamlaka ya kutoa taarifa za kurudia rudia na kukanusha kuwa wananchi waliokuwa wakiandamana siyo wanachama wa chama hicho bali ni mamluki, huku akijigamba kuwa chama hicho kitashinda kwa vishindo na kwamba vitisho vya kuandamana havitasaidia.
Aidha, alisema wanachama wa kijiji cha Luhindo hawakupiga kura za maoni bali yalikuwa ni mapendekezo tu ya kuchagua nani anayefaa kuwa mwenyekiti wa kijiji na kuna vigezo vingi vinavyoangaliwa na chama na kwamba siyo lazima warudishe jina lililopata kura nyingi za maoni kwa kuwa viongozi wanapimwa na vigezo vingi na siyo tu wingi wa kura.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment