Seif alipua ubadhirifu viongozi wa CCM, Serikali

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ni wabadhilifu wa fedha za umma wakihusishwa katika kashfa mbalimbali hali ambayo inachangia kuongeza umaskini kwenye jamii.

Kashfa hizo ni pamoja na wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mkataba wa Ridhmond, ununuzi wa rada, Escrow, mikataba mibovu ya madini, ujunzi wa minara pacha.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye Viwanja vya Mashujaa, mkoani Mtwara.

Alisema CCM imeshindwa kuisimamia Serikali ili kukomesha vitendo hivyo ambapo viongozi wa mikoa ya Kusini wakiwemo wabunge wanaotokana na chama hicho hawana uzalendo.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, aliwataka wakazi wa mikoa hiyo ukiwemo

Mtwara, kubadilisha mfumo wa uongozi kwa kuiondoa CCM madarakani ili waweze kupata maendeleo.

Alisema kama CCM itaondoka madarakani, wakazi wa Mtwara watapata maendeleo, kunufaika na rasirimali zilizopo kama bahari, kilimo cha korosho, ufuta, Gesi na Hifadhi ya Wanyama Selous.

"Kimsingi nashangazwa na hali nguvu za maisha kwa wakazi wa mikoa ya Kusini wakati imebahatika kuwa na rasirimali nyingi na maliasili za kutosha.

"Hakuna sababu ya kuishi maisha magumu bali nchi yetu ina tatizo la uongozi ambao ambao chanzo chake ni kukosa mfumo madhubuti...nchi imekuwa kinara wa ukiukwaji wa haki za binadamu ambapo leo hii, vijana hapa Mtwara hawana ajira mbali ya rasirimali zilizopo," alisema.

Aliongeza kuwa, vijana hao wanpokwenda jijini Dar es Salaam wanabadilishwa jina na kuitwa "Machinga" hivyo kwa hali ilivyo sasa, ipo haja ya kubadilisha mfumo wa uongozi.

Maalim Seif alisema CUF wapo tayari kupokea jukumu la kujenga uchumi wa nchi kupitia rasilimali na maliasili zilizopo kwani chama hicho kina dhamira ya kuwakomboa wananchi katika lindi la umaskini na kushiriana nao ili kuijenga nchi.

"CUF kimekusudia kubadilisha mfumo wa halmashauri zetu uliopo sasa na kuanzisha mfumo mpya ili halmashauri ziweze kujikita zaidi katika kusimamia shughuli zitazokuza uchumi kupitia kilimo cha kisasa, kuanzisha viwanda vya kati na vidogovidogo vitavyoendeshwa kwa kutumia malighafi za kilimo hivyo kuongeza ajira kwa vijana," alisema.

Katika ziara hiyo ambayo inaendelea mkoani humo kwenye Wilaya za Tandahimba, Newala na kumalizia Tunduru, mkoani Ruvuma, Maalim Seif ameongozana na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Bw. Abdul Kambaya.

- Majira

Post a Comment

Previous Post Next Post