CHAMA cha Wananchi (CUF),
kimesema baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ni
wabadhilifu wa fedha za umma wakihusishwa katika kashfa mbalimbali hali
ambayo inachangia kuongeza umaskini kwenye jamii.
Kashfa hizo ni pamoja na wizi wa fedha
kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mkataba wa Ridhmond, ununuzi wa
rada, Escrow, mikataba mibovu ya madini, ujunzi wa minara pacha.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif
Sharif Hamad, aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi
kwenye Viwanja vya Mashujaa, mkoani Mtwara.
Alisema CCM imeshindwa kuisimamia Serikali
ili kukomesha vitendo hivyo ambapo viongozi wa mikoa ya Kusini wakiwemo
wabunge wanaotokana na chama hicho hawana uzalendo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, aliwataka wakazi wa mikoa hiyo ukiwemo
Mtwara, kubadilisha mfumo wa uongozi kwa kuiondoa CCM madarakani ili waweze kupata maendeleo.
Alisema kama CCM itaondoka madarakani,
wakazi wa Mtwara watapata maendeleo, kunufaika na rasirimali zilizopo
kama bahari, kilimo cha korosho, ufuta, Gesi na Hifadhi ya Wanyama
Selous.
"Kimsingi nashangazwa na hali nguvu za
maisha kwa wakazi wa mikoa ya Kusini wakati imebahatika kuwa na
rasirimali nyingi na maliasili za kutosha.
"Hakuna sababu ya kuishi maisha magumu bali
nchi yetu ina tatizo la uongozi ambao ambao chanzo chake ni kukosa mfumo
madhubuti...nchi imekuwa kinara wa ukiukwaji wa haki za binadamu ambapo
leo hii, vijana hapa Mtwara hawana ajira mbali ya rasirimali zilizopo,"
alisema.
Aliongeza kuwa, vijana hao wanpokwenda
jijini Dar es Salaam wanabadilishwa jina na kuitwa "Machinga" hivyo kwa
hali ilivyo sasa, ipo haja ya kubadilisha mfumo wa uongozi.
Maalim Seif alisema CUF wapo tayari kupokea
jukumu la kujenga uchumi wa nchi kupitia rasilimali na maliasili
zilizopo kwani chama hicho kina dhamira ya kuwakomboa wananchi katika
lindi la umaskini na kushiriana nao ili kuijenga nchi.
"CUF kimekusudia kubadilisha mfumo wa
halmashauri zetu uliopo sasa na kuanzisha mfumo mpya ili halmashauri
ziweze kujikita zaidi katika kusimamia shughuli zitazokuza uchumi
kupitia kilimo cha kisasa, kuanzisha viwanda vya kati na vidogovidogo
vitavyoendeshwa kwa kutumia malighafi za kilimo hivyo kuongeza ajira kwa
vijana," alisema.
Katika ziara hiyo ambayo inaendelea mkoani
humo kwenye Wilaya za Tandahimba, Newala na kumalizia Tunduru, mkoani
Ruvuma, Maalim Seif ameongozana na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na
Mahusiano ya Umma, Bw. Abdul Kambaya.
- Majira
إرسال تعليق