Serikali yaipongeza Tusiime kuingia kumi bora kitaifa

Serikali yaipongeza Tusiime kuingia kumi bora kitaifa 
SERIKALI  imeipongeza shule ya Tusiime kwa kuwa shule pekee kutoka Mkoa wa Dar es salaam iliyoingia kwenye kumi bora kitaifa na kufaulisha wafunzi wote  168 kwa alama A na kuongoza katika mkoa wa Dar es salaam na wilaya ya Ilala.
Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Bernadetha Thomas, wakati wa mahafali ya kumaliza shule ya msingi na awali Tusiime Tabata jijini Dar es Salaam, ambayo ndiyo pekee katika shule kumi bora yenye wanafunzi zaidi ya 100 kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka huu.
“Nasema hivyo kwa sababu shule hii ni miongoni mwa shule bora nchini, na kama mnavyojua matokeo ya mitihani ya taifa yanadhihirisha hili…tunapozungumzia mafanikio ya shule hii, tunamaanisha juhudi zenu wazazi na wafanyakazi wote wa Tusiime.
“ Nimefarijika sana  kusikia uongozi wa shule unajali maslahi ya wafanyakazi, hilo ni jambo jema kwa sababu wao ndio wazalishaji wakuu na ndio watenda kazi, kujali maslahi yao na kuwapa motisha ni kuongeza tija na hatimaye ufanisi….kuna baadhi ya wawekezaji katika sekta ya elimu hujali zaidi faida bila kujali maslahi ya mzalishaji wa faida hiyo,” alisema.
Aidha aliwapongeza wamiliki wa shule hiyo kwa uamuzi wao wa busara kuwekeza kwenye elimu na kwamba uamuzi wao umepanua wigo wa fursa za elimu nchini na kuchangia ukuaji.
Awali katika risala yake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Philbert Simon, alisema shule yake imetimiza miaka 15 yenye mafanikio katika taaluma  na nje ya taaluma na aliahidi  wataendelea kufanya hivyo kwa kuongeza bidii na maarifa zaidi katika kazi zao ili kuzalisha raia mahiri na wenye tija kwa taifa.
Alisema mafanikio yao yametokana na kuwa na timu nzuri ya wanataaluma wanaokidhi viwango na kujituma .
“Katika kutekeleza matokeo makubwa sasa (BRN) shule yetu imesimamia kwenye rangi ya kijani ambayo ndio kielelezo cha ushindi wa juu kabisa. Tutatumia raslimali na uwezo wetu wote tuliojaliwa kuhakikisha tunailinda nafasi hiyo,” alisema Simon.

Post a Comment

Previous Post Next Post