![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjGE2xqKeDJhdn_8iAR91QJmQuKBibeh9r1-iuZOkwKmwnDtb3SouDIITGQ7aH60_78Qe8wfcm92qgYCwnYh1MKLLBM5OAjOULjKeEnxgQ75MtG-QQAiXwdf8ybobQkqaHU3eqCc3B5hUni/s1600/SPIKA.jpg)
Ingawa harakati hizo zimeanzia mbali, kwa wanawake kutaka kufanya mambo sawa na wanaume na kuona ndoto zao zinatimia katika maisha yao, leo zimekuwa kweli, kwani mafanikio ya uwiano ni makubwa.
Jambo la muhimu ni kwamba, mafanikio ambayo yamepatikana ni mazao ya kuamua kwa ujasiri na kuweka nia thabiti.
Leo nitawaangazia baadhi ya wanawake waliofanya vizuri na kupata mafanikio makubwa hapa nchini.
Julieth Kairuki
Ni Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza mwanamke katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), katika uteuzi uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete.
Mwanamama huyu, ana shahada ya uzamili ya sheria, akiwa mtalamu wa ubia kati ya serikali na watu binafsi.
Amepita sehemu mbalimbali ikiwemo Chama cha Mabenki ya Afrika Kusini.
Sauda Rajabu
Ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ndege ya Precision Air.
Alianza kutumikia nafasi hiyo kutoka kwa Alfonce Kioko aliyemaliza muda wake.
Ana shahada ya kwanza ya biashara na amewahi kufanya kazi katika mashirika mengine ya ndege likiwemo Kenya Airways.
Anne Makinda
NI mwanamke wa kwanza nchini kuwa Spika wa Bunge la Muungano, akichukua nafasi hiyo kutoka kwa Samuel Sitta.
Makinda, amevunja rekodi kwa kukaa bungeni kwa miaka mingi kwani alianza kuwa Mbunge wa Njombe mwaka 1975 hadi leo akiwa ni Mbunge wa Njombe Kusini.
Balozi Liberata Mulamula
Ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico. Amewahi kuwa balozi Canada kuanzia mwaka 1999 hadi 2002.
Pia, alishawahi kuteuliwa kuwa mmoja wa wasuluhishi wa mgogoro wa Rwanda. Ni msomi mwenye shahada ya uzamili ya sanaa aliyosomea Chuo Kikuu cha St. John’s, Marekani mwaka 1989.
Mchungaji Getrude Rwakatare
Huyu ni Mchungaji na kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God na mwanzilishi wa shule za St. Mary’s International mwaka 1997.
Licha ya kazi ya kuhubiri Injili, Mama Rwakatare ana chombo cha habari ambacho ni Praise Power Radio 99.2 FM, lakini pia ni mbunge wa viti maalum (CCM).
Getrude Mongella
Alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Bunge la Afrika, amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini India kuanzia mwaka 1991 hadi 1992 na akawa Katibu katika Mkutano wa Wanawake Duniani uliofanyika Beijing China mwaka 1995.
Aliwahi kuwa mshauri wa Mkurugenzi Mkuu wa Unesco na aliwatumikia wananchi wa Ukerewe akiwa mbunge kuanzia 2000 hadi 2010 na Februari mwaka 2008, alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya African Press Organization (APO).
Halima Mdee
Huyu ni mbunge kijana ambaye baada ya kuwa mbunge wa Viti Maalumu kwa miaka mitano, aliamua kupambana jimboni kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 na kufanikiwa kukinyakua kiti cha Kawe jijini Dar es Salaam.
Pia mwaka huu, alifanikiwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama kikuu cha upinzani nchini CHADEMA, (BAWACHA Taifa).
Asha-Rose Migiro
Asha-Rose Migiro ni mwanasheria na mwanasiasa. Licha ya kufundisha sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mama huyu aliwahi kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania.
Lakini kikubwa zaidi, ni pale alipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Juni 2012 na sasa mwanamama huyu ni Mbunge wa viti maalum (CCM), na Waziri wa Sheria na Katiba.
Susan Mashibe
Huyu ni rubani na mhandisi wa ndege, akiwa mwanamke wa kwanza nchini kuwa na taaluma hizo alizopatia Chuo Kikuu cha Michigan, Marekani. Ni Mwanzilishi na kiongozi wa Tanzanite Jet Centre Ltd, kampuni aliyoianzisha mwaka 2003, ambayo sasa inajulikana kama Via Aviation na inajishughulisha na biashara ya mambo ya anga nchini na barani Afrika.
Judith Wambura ‘Lady Jaydee’
Ni msanii mwenye heshima Tanzania, amepata mafanikio katika kazi zake za muziki na kuweza kuwa mfano wa kuigwa kwa wasanii wengine kutokana na uchapakazi wake.
Anamiliki mgahawa, magari ya kifahari, bendi ya muziki ‘Machozi Band’ na alishawahi kuanzisha maji yake ya Jaydee ambayo yalizuiwa.
Joyce Mhavile
Ni Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha ITV na Radio One kuanzia mwaka 1994.
Mwanamama huyu amefanikiwa kukiongoza kituo hicho cha runinga na radio hadi kushika nafasi ya kwanza kwa ufanisi mwaka jana.
Amebobea kwenye taaluma ya uandishi wa habari na ni mmoja wa wanawake mahiri wenye mafanikio na kuwa mfano kwa wasichana wanaochipukia.
- Tanzania Daima
Post a Comment