Wadau wakosoa utendaji wa serikali kwa utoroshwaji watoto 144

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu
Wadau wa masuala ya haki za binadamu wa mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini, wamekosoa utendaji wa serikali, mkoani Kilimanjaro kwa kushindwa kuwashughulikia watu wanaodaiwa kuwatorosha watoto 144 wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao wamewekwa kinyumba na wengine kupelekwa kufanya kazi kwenye miji mbalimbali nchini.
Mratibu wa kampeni ya siku 16 ya Kupambana na Ukatili wa Kijinsia katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga, Hillary Tesha, alisema jana kuwa wakati serikali ikiwa imetoa mwongozo wa kisera wa sekta ya afya wa kuzuia na kupambana na ukatili huo wenye lengo la

kukabiliana na changamoto hiyo, jumla ya watoto 127 waliripotiwa katika vituo vya polisi huku wanafunzi 17 wakikatishwa masomo yao kwa kutoroshwa na kuwekwa kinyumba katika mkoa wa Kilimanjaro, kati ya mwezi Januari hadi Novemba mwaka huu.

“Kinara wa matukio haya ya ukatili na ulevi wa kupindukia ni Wilaya ya Rombo ambapo takwimu zetu zinaonyesha kwamba watu waliobakwa, walikuwa 123, matukio ya ulawiti yapo 31, ya kutorosha watoto 127 na wanafunzi 17.

Sisi wadau tunamuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini  (IGP), Ernest Mangu kuyaimarisha madawati ya jinsia yaliyoanzishwa katika vituo mbalimbali vya Polisi kwa kuona haja ya kutoa mafunzo, kuongeza rasilimali watu na fedha ili kuleta ufanisi katika kukabiliana na ukatili unaoendelea,”alisema Hillary.

Aliiomba serikali kudhibiti kasi ya kuenea kwa pombe kali zisizo na viwango ambazo zinachangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia miongoni mwa wakazi wa mikoa hiyo ya Kaskazini.

Hata hivyo, Mkuu wa Dawati la Jinsia la Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Lyimo, aliiambia NIPASHE kuwa katika matukio ya ubakaji kwa kipindi kisichozidi miezi 10, wamefanikiwa kuwafikisha mahakamani watu 92 ambapo kesi 78 kati yake zimeamuliwa na mahakama huku kesi tatu pekee zikiwa zimefanikiwa kutoa fundisho kwa watu waliobainika kufanya makosa hayo.

Maadhimisho hayo yanaratibiwa na Shirika la Haki za Binadamu na Jinsia mkoani Kilimanjaro (KWIECO), ikishirikiana na Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji pamoja na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia (NAFGEM), Kikundi cha Wanawake cha Kupambana na Ukimwi (KIWAKUKI), Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF Net), Twaweza na hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post