KATIKA
hali isiyo ya kawaida, Bunge jana liliahirishwa ghafla jioni baada ya
Serikali kuamua kuundoa Muswada wa Sheria ya Takwimu.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, alisema Serikali imeomba kuondoa muswada huo ili kuufanyia maboresho.
“Waheshimiwa Wabunge, Serikali imeamua kuondoa muswada huo ili
kuufanyia maboresho. Kwa hali hii naahirisha Bunge hadi kesho, saa tatu
asubuhi,” alisema na kuahirisha Bunge.
Nje ya Bunge, Mpina aliwaambia wanahabari kuwa, baada ya kupata maoni
ya waandishi kuhusu ubaya wa sheria hiyo, aliongea na Waziri wa Fedha
na huenda mazungumzo hayo yamechangia kuahirisha Bunge.
Awali jana asubuhi, Serikali ilipendekeza kuwa mtu au chombo chochote
cha habari kitakachochapisha takwimu za uongo au bila idhini ya
Mtakwimu Mkuu, kifungo jela mwaka mmoja.
Pendekezo hilo ambalo pia linazuia taasisi binafsi zilizokuwa
zikikusanya na kutangaza takwimu za tafiti mbalimbali nchini bila
idhini, lilitolewa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, wakati
akiwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Takwimu.
Kwa mujibu wa muswada huo, takwimu rasmi ni zile zitakazotolewa na ofisi, taasisi za serikali na wakala wake.
Wakati Serikali ikija na rungu hilo kwa tasnia ya habari, Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luaga
Mpina, amependekeza adhabu hiyo iongezwe kutoka miezi 12 hadi miaka
mitatu.
Akiwasilisha muswada huo Bungeni jana, Waziri Mkuya alisema ibara ya
37 (4) inapendekeza adhabu kwa vyombo vya habari vitakavyochapisha
taarifa za kitakwimu za uongo au za upotoshwaji iwe miezi 12.
Alisema sheria hiyo itasaidia sana kujenga nidhamu ya utoaji taarifa za kitakwimu.
Kambi ya upinzani yapinga
Kambi Rasmi ya Upinzani, kupitia msemaji wake, James Mbatia, imepinga
vikali sheria hiyo kwani itaendelea kuminya uhuru wa habari nchini.
Mbatia, alisema kwa muda mrefu sasa wanahabari na vyombo vya habari
vimekuwa vikihitaji uhuru wa habari na wanahabari, lakini Serikali
imekuja na sheria inayominya zaidi uhuru huo.
Alisema pamoja na serikali kuingilia uhuru wa habari na vyombo vya
habari pasipo kuzingatia sheria, ni vibaya zaidi kwa sasa Bunge kutunga
sheria ya kuendelea kuminya uhuru wa habari.
“Swali la kujiuliza, je ni nani atakayethibitisha uongo au upotoshaji
wa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari? Je haitakuwa kwamba
taarifa zisizoipendeza serikali ndio zitaonekana za upotoshaji hata kama
zina ukweli,?” alihoji Mbatia.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi taifa,
alisema kuwa taaluma ya habari inazingatia utafiti na si rejea pekee ya
taarifa rasmi zilizotolewa na serikali, hivyo kuvibana kutumia taarifa
za serikali na wakala wake ni kutotambua kazi ya wanahabari ya kufanya
tafiti na kuitaarifu jamii juu ya mambo yanayohusu jamii.
Alisema hatua hiyo mbaya ni mwendelezo wa Serikali kuvinyima uhuru
vyombo vya habari na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari kwa mujibu
wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbatia, alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inashauri kuwa
muswada huo uainishe aina ya takwimu ambazo ni lazima zitolewe na
Mtakwimu Mkuu wa serikali au Idara na taasisi tajwa, kwani ni dhahiri
kwamba aina za takwimu hutofautiana kwa wakati, umuhimu na mazingira.
Kwa hali hiyo, alisema si lazima takwimu zote zinazoihusu nchi
zitolewe na serikali pekee na kutolea mfano wa takwimu zinazohusu
matukio mbalimbali nchini kwamba, haziwezi kutolewa na serikali kwa
kuzingatia uwezo, weledi na utendaji wa serikali hii ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
“Mheshimiwa Spika, ibara ya 37 (4) inazungumzia makosa na adhabu kwa
vyombo vya habari, mojawapo ya adhabu hizo ikiwa ni kifungo cha jela
(Imprisonment). Pamoja na kuminya uhuru wa vyombo vya habari bado
haielezwi ni kwa vipi chombo cha habari kitapelekwa jela, kwa tafsiri
ndogo ni kwamba bado hakuna uzoefu wa utekekelezaji wa kutoa adhabu ya
aina hiyo kwa chombo cha habari,” alisema Mbatia.
Alisema kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka serikali kurejea
upya muswada huo kwa kutokuwa na hila na vyombo vya habari na kuangalia
mbali zaidi kwa manufaa ya taifa.
Mbali na kulalamikia kuminywa kwa uhuru wa habari, Mbatia alisema
ibara ya 20 inatamka kuwa, takwimu rasmi ni zile zitakazotolewa na
serikali na wakala zake, bila kuzingatia kuwa kuna taasisi zenye weledi
na uwezo wa kiwango cha juu wa kutoa takwimu sahihi kwa mustakabali wa
maendeleo ya nchi.
Alisema kuna takwimu aidha kwa makusudi au kwa udhaifu wake, haziwezi
kutolewa na Serikali na kutolea mfano wa takwimu za mauaji ya raia,
umaskini, takwimu za uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo, takwimu
za uzalishaji wa mazao ya mifugo na takwimu za uvunjifu wa haki za
binadamu.
Alisema kuwa takwimu hizi zimekuwa zikipatikana katika taasisi
binafsi hususani kituo cha sheria na haki za binadamu, taasisi ya
‘Economic and Social Research Foundation’ na ‘Research and Poverty
Alleviation’, asasi za kiraia, taasisi za Kidini na kadhalika.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka serikali kuweka sheria ya
kutambua takwimu hizi ambazo zitajenga serikali yenye nidhamu ya
uwajibikaji kwa wananchi na sio kuficha uovu kwa kutunga sheria
kandamizi kwa taasisi za kuwasaidia wanyonge,” alisema.
Akizungumzia ibara ya 18 (2), Mbatia alisema kipengele hicho kinatoa
mamlaka kwa mkurugenzi mkuu pekee kutoa kibali cha ukusanyaji wa takwimu
rasmi, kitu ambacho kinanyima uhuru wa taasisi binafsi na watu binafsi
kukusanya takwimu mbalimbali.
“Mheshimiwa Spika, ibara ya 18 (2) inasomeka, “bila kujali masharti
yaliyomo katika sheria nyingine yoyote hakuna mtu au wakala anayeweza
kuidhinisha kuanza au kuanzisha ukusanyaji wa takwimu rasmi isipokuwa
kwa idhini ya Mkurugenzi Mkuu.
“ Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inatambua kuwa
wanafunzi wa shahada ya pili na tatu hufanya tafiti mbalimbali hususani
za kitakwimu, ambapo sasa watahitajika kupata kibali kwa Mtakwimu Mkuu
ili takwimu zao ziwe halali, pili taasisi binafsi hukusanya takwimu
ambazo serikali haizikusanyi kwa makusudi mfano takwimu za mauaji
yanayofanywa na Jeshi la Polisi kwa raia, ambapo ofisi ya mtakwimu mkuu
haijawahi kutoa takwimu hizi kwa watanzania ili waweze kujua ukweli wa
mambo hayo na pia kupata haki yao ya kupata habari juu ya utendaji na
uvunjifu wa haki za binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi nchini, na
sasa tunatunga sheria ya kulinda uovu wa vyombo hivi,”.
“Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni inalitaka bunge kutunga sheria
zitakazoiwajibisha serikali, wawajibisha watendaji wabovu, kukomeza
ukandamizaji na kujenga jamii na viongozi wenye kuwajibika kwa umma na
sio kujenga jamii ya kulindana na kuwafanya wengine waishi kwa hofu
kutokana na sheria kutotambua wajibu wa kazi zao katika jamii. Hivyo
basi bunge lina nafasi ya kuhakikisha kuwa taasisi mbalimbali za binafsi
na kijamii zinaruhusiwa kufanya tafiti za kitakwimu na kuweza kutoa
taarifa zake kwa utaratibu wenye tija kwa taifa,” alisema.
Tanzania Daima

Post a Comment