Serikali yang’oa muswada ghafla

Serikali yang'oa muswada ghafla
  • Ulikuwa unaweka kitanzini uhuru wa habari

KATIKA hali isiyo ya kawaida, Bunge jana liliahirishwa ghafla jioni baada ya Serikali kuamua kuundoa Muswada wa Sheria ya Takwimu.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, alisema Serikali imeomba kuondoa muswada huo ili kuufanyia maboresho.
“Waheshimiwa Wabunge, Serikali imeamua kuondoa muswada huo ili kuufanyia maboresho. Kwa hali hii naahirisha Bunge hadi kesho, saa tatu asubuhi,” alisema na kuahirisha Bunge.
Nje ya Bunge, Mpina aliwaambia wanahabari kuwa, baada ya kupata maoni ya waandishi kuhusu ubaya wa sheria hiyo, aliongea na Waziri wa Fedha na huenda mazungumzo hayo yamechangia kuahirisha Bunge.
Awali jana asubuhi, Serikali ilipendekeza kuwa mtu au chombo chochote cha habari kitakachochapisha takwimu za uongo au bila idhini ya Mtakwimu Mkuu, kifungo jela mwaka mmoja.
Pendekezo hilo ambalo pia linazuia taasisi binafsi zilizokuwa zikikusanya na kutangaza takwimu za tafiti mbalimbali nchini bila idhini, lilitolewa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, wakati akiwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Takwimu.
Kwa mujibu wa muswada huo, takwimu rasmi ni zile zitakazotolewa na ofisi, taasisi za serikali na wakala wake.
Wakati Serikali ikija na rungu hilo kwa tasnia ya habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luaga Mpina, amependekeza adhabu hiyo iongezwe kutoka miezi 12 hadi miaka mitatu.
Akiwasilisha muswada huo Bungeni jana, Waziri Mkuya alisema ibara ya 37 (4) inapendekeza adhabu kwa vyombo vya habari vitakavyochapisha taarifa za kitakwimu za uongo au za upotoshwaji iwe miezi 12.
Alisema sheria hiyo itasaidia sana kujenga nidhamu ya utoaji taarifa za kitakwimu.
Kambi ya upinzani yapinga
Kambi Rasmi ya Upinzani, kupitia msemaji wake, James Mbatia, imepinga vikali sheria hiyo kwani itaendelea kuminya uhuru wa habari nchini.
Mbatia, alisema kwa muda mrefu sasa wanahabari na vyombo vya habari vimekuwa vikihitaji uhuru wa habari na wanahabari, lakini Serikali imekuja na sheria inayominya zaidi uhuru huo.
Alisema pamoja na serikali kuingilia uhuru wa habari na vyombo vya habari pasipo kuzingatia sheria, ni vibaya zaidi kwa sasa Bunge kutunga sheria ya kuendelea kuminya uhuru wa habari.
“Swali la kujiuliza, je ni nani atakayethibitisha uongo au upotoshaji wa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari? Je haitakuwa kwamba taarifa zisizoipendeza serikali ndio zitaonekana za upotoshaji hata kama zina ukweli,?” alihoji Mbatia.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi taifa, alisema kuwa taaluma ya habari inazingatia utafiti na si rejea pekee ya taarifa rasmi zilizotolewa na serikali, hivyo kuvibana kutumia taarifa za serikali na wakala wake ni kutotambua kazi ya wanahabari ya kufanya tafiti na kuitaarifu jamii juu ya mambo yanayohusu jamii.
Alisema hatua hiyo mbaya ni mwendelezo wa Serikali kuvinyima uhuru vyombo vya habari na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbatia, alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inashauri kuwa muswada huo uainishe aina ya takwimu ambazo ni lazima zitolewe na Mtakwimu Mkuu wa serikali au Idara na taasisi tajwa, kwani ni dhahiri kwamba aina za takwimu hutofautiana kwa wakati, umuhimu na mazingira.
Kwa hali hiyo, alisema si lazima takwimu zote zinazoihusu nchi zitolewe na serikali pekee na kutolea mfano wa takwimu zinazohusu matukio mbalimbali nchini kwamba, haziwezi kutolewa na serikali kwa kuzingatia uwezo, weledi na utendaji wa serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mheshimiwa Spika, ibara ya 37 (4) inazungumzia makosa na adhabu kwa vyombo vya habari, mojawapo ya adhabu hizo ikiwa ni kifungo cha jela (Imprisonment). Pamoja na kuminya uhuru wa vyombo vya habari bado haielezwi ni kwa vipi chombo cha habari kitapelekwa jela, kwa tafsiri ndogo ni kwamba bado hakuna uzoefu wa utekekelezaji wa kutoa adhabu ya aina hiyo kwa chombo cha habari,” alisema Mbatia.
Alisema kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka serikali kurejea upya muswada huo kwa kutokuwa na hila na vyombo vya habari na kuangalia mbali zaidi kwa manufaa ya taifa.
Mbali na kulalamikia kuminywa kwa uhuru wa habari, Mbatia alisema ibara ya 20 inatamka kuwa, takwimu rasmi ni zile zitakazotolewa na serikali na wakala zake, bila kuzingatia kuwa kuna taasisi zenye weledi na uwezo wa kiwango cha juu wa kutoa takwimu sahihi kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi.
Alisema kuna takwimu aidha kwa makusudi au kwa udhaifu wake, haziwezi kutolewa na Serikali na kutolea mfano wa takwimu za mauaji ya raia, umaskini, takwimu za uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo, takwimu za uzalishaji wa mazao ya mifugo na takwimu za uvunjifu wa haki za binadamu.
Alisema kuwa takwimu hizi zimekuwa zikipatikana katika taasisi binafsi hususani kituo cha sheria na haki za binadamu, taasisi ya ‘Economic and Social Research Foundation’ na ‘Research and Poverty Alleviation’, asasi za kiraia, taasisi za Kidini na kadhalika.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka serikali kuweka sheria ya kutambua takwimu hizi ambazo zitajenga serikali yenye nidhamu ya uwajibikaji kwa wananchi na sio kuficha uovu kwa kutunga sheria kandamizi kwa taasisi za kuwasaidia wanyonge,” alisema.
Akizungumzia ibara ya 18 (2), Mbatia alisema kipengele hicho kinatoa mamlaka kwa mkurugenzi mkuu pekee kutoa kibali cha ukusanyaji wa takwimu rasmi, kitu ambacho kinanyima uhuru wa taasisi binafsi na watu binafsi kukusanya takwimu mbalimbali.
“Mheshimiwa Spika, ibara ya 18 (2) inasomeka, “bila kujali masharti yaliyomo katika sheria nyingine yoyote hakuna mtu au wakala anayeweza kuidhinisha kuanza au kuanzisha ukusanyaji wa takwimu rasmi isipokuwa kwa idhini ya Mkurugenzi Mkuu.
“ Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inatambua kuwa wanafunzi wa shahada ya pili na tatu hufanya tafiti mbalimbali hususani za kitakwimu, ambapo sasa watahitajika kupata kibali kwa Mtakwimu Mkuu ili takwimu zao ziwe halali, pili taasisi binafsi hukusanya takwimu ambazo serikali haizikusanyi kwa makusudi mfano takwimu za mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi kwa raia, ambapo ofisi ya mtakwimu mkuu haijawahi kutoa takwimu hizi kwa watanzania ili waweze kujua ukweli wa mambo hayo na pia kupata haki yao ya kupata habari juu ya utendaji na uvunjifu wa haki za binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi nchini, na sasa tunatunga sheria ya kulinda uovu wa vyombo hivi,”.
“Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni inalitaka bunge kutunga sheria zitakazoiwajibisha serikali, wawajibisha watendaji wabovu, kukomeza ukandamizaji na kujenga jamii na viongozi wenye kuwajibika kwa umma na sio kujenga jamii ya kulindana na kuwafanya wengine waishi kwa hofu kutokana na sheria kutotambua wajibu wa kazi zao katika jamii. Hivyo basi bunge lina nafasi ya kuhakikisha kuwa taasisi mbalimbali za binafsi na kijamii zinaruhusiwa kufanya tafiti za kitakwimu na kuweza kutoa taarifa zake kwa utaratibu wenye tija kwa taifa,” alisema.
Tanzania Daima

Post a Comment

أحدث أقدم