Tunasikitishwa na namna ambavyo serikali imekuwa
ikishughulikia suala laupungufu wa dawa na vifaa tiba nchini. Siku za karibuni,
kumekuwepo na taarifa za ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika sehemu mbalimbali
nchinilakini serikali bado haijachukua hatua madhubuti, jambo ambalo linaweza
kuchangia wagonjwa kuteseka zaidi na hata kusababisha vifo.
Sikika ilitegemea serikali
ingeangalia janga hili kwa makini zaidi na kulipa mara moja deni lote (Tshs
bilioni 90),linalodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa(MSD). Badala yake ni Tshs.
bilioni 20 tu zilizotolewa mpaka sasa na nyingine Tsh bilioni 11 zilizoahidiwa
kutolewa ndani ya mwezi mmoja.Kutokana na unyeti wa suala hili ambalo linagusa
maisha ya wananchi, tungependa kuona serikali ikilipa fedha zote inayodaiwa na
MSD ili kuiwezesha kufanya kazi ipasavyo na kupunguza upungufu wa dawa na vifaa
tiba uliojitokeza nchini.
Deni la MSD lilitakiwa kulipwa tangu kitambo na
mikakati ya kuzuia ongezekola deni hilo ilitakiwa iwepo na itekelezwe. Mara
nyingi na kwa nyakati tofauti tofauti wabunge, hususani Kamati ya Kudumu ya
Huduma za Jamii wamekuwa wakiitaka Serikali kuilipa MSD deni linalodaiwa.Tunaamini
kwamba hali iliyopo sasa ingeweza kuzuilika kama Serikali ingesikiliza na
kufanyia kazi maagizo ya Bunge kwa wakati. Badala yake, deni limekuwa
likiongezeka huku mikakati ya kulipa deni hilo ikiwa haina tija.
Tatizo la uhaba wa dawa na vifaa tiba linaloendelea kwa sasa linasababishwa na
kukua kwa deni na hivyo kuifanya MSD kushindwa kusambaza dawa na vifaa tiba
kwa vituo vya kutolea huduma vyenye
madeni.Hata hivyo, tatizo la upungufu wa dawa na vifaa tiba nchini ni sugu na
linapaswa kutatuliwa. Sababu kuu zinazosababisha uhaba wa dawa nchini ni bajeti
ndogo inayotengwa, ucheleweshaji katika kutoa fedha zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi
wa dawa pamoja na takwimu zisizo sahihi juu ya mahitaji halisi ya dawa nchini.
Hivyo, ni vyema Serikali ikatatua pia vyanzo vingine vinavyosababisha uhaba wa
dawa nchini pamoja na kulipa deni kamili.
Kwa mfano, katika hospitali ya Sinza Palestina, walikuwa
wakidaiwa na MSDTsh. milioni 93. Oktoba mwaka huu, walipokea fedha kutoka Mfuko
wa Afya wa pamoja (health basket fund) na kuagiza MSD dawa na vifaa tiba vyenye
gharama ya Tsh. milioni 100. Hata hivyo, walipokea mzigo wenye thamani ya Tsh.
milioni 25 tu kwa sababu MSD walikata deni wanalowadai la Tsh. milioni 75. Hii imelazimisha
hospitali hiyo kutumia dawa walizopokea kwa ajili ya dharura tu, kwa sababu
dawa hizo haziwezi kukidhi mahitaji yao ambapo wanahudumia takribani wagonjwa
600 kwa siku, hivyo kusababisha uhaba wa dawa katika hospitali hiyo, kama
ambavyo imekuwa ikiripotiwa na vyombo vya habari.
Hali hii katika hospitali ya Sinza Palestina
inafanana na hospitali nyingi nchini.Ni wakati muafaka sasa wa Serikali kuhakikisha
tatizo la uhaba wa dawa na vifaa tiba nchinilinakwisha na kubaki kuwa historia.
Sikika inatoa wito kwaSerikali kufanya jitihada za
makusudi katika kumaliza tatizo hili sugu la uhaba wa dawa katika vituo vya huduma
za afya kwa kushughulikia mzizi wa tatizo na si kusubiri kutatuamatatizo
yanayoibuka mara kwa mara.Hivyo basi, Sikika inashauri bajeti ya dawa iongezwe
kufikia angalau nusu ya mahitaji ya nchi, ambayo ni Tsh.bilioni 250 kwa mwaka. Pia
tunashauri kuwa Wizara ya Fedha na Uchumi (MoFEA)kutoa gawio la fedha zote zinazotengwa
kwa ajili ya dawa na vifaa tiba kwa mkupuo mmoja kwenda kwenye akaunti za vituo
MSD.Gawio hilo litolewe mwanzo wa mwaka ili kuiwezesha MSD kununua dawa hizo
kwa wakati.
Pia tunaitaka MSD kuimarisha mfumo mzima wa ununuzi
na usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini kwa kuhakikisha kuwa hakuna upungufu
katika maghala yao. Ni vema MSD ikaondokana na kuchelewa kwa usambazaji wa dawa
kwenye vituo vya kutolea huduma na kuimarisha mfumo wa kufidia pale ambapo dawa
zimekosekana au kutolewa katika idadi ndogo. Mwisho, MSDiboreshe utendaji wa
kazi, uwazi na uwajibikaji kwa sababu hizo ndizo nguzo borakatika mfumo wa ununuzi
na usambazaji wa dawa .
Sikika ingependa pia kuelimisha tena umma kuwa
kusitishwa kwa misaada ya fedha na wahisani ni kwenye bajeti ya maendeleo tu na
sio kwenye mfuko wa pamoja wa afya (Health
Basketi Fund) kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa na baadhi ya watu. Mfuko wa
pamoja wa afya unaotolewa na wahisani kwenye halmashauri, theluthi ya fedha
hizo zinapaswa kutumika katika ununuzi ya dawa muhimu na vifaa tiba.
Mwisho, Sikika inapenda kuwapongeza Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii Dr. Seif Rashid na Katibu Mkuu wake Dr. Donan Mmbando kwa
kutoa tamko la kusitisha kutumika kwa viwango vipya vya gharama za matibabu
katika hospitali ya taifa ya Muhimbili. Gharama hizi mpya si kwamba
zingewanyiwa wananchi walio wengi haki ya kupata huduma bora za afya bali pia si
sahihi kuwalipisha zaidi wagonjwa ili
kulipa deni ambalo hawakuhusika nalo.
Mr. Irenei Kiria,
Executive Director of Sikika,
P. O. Box 12183 Dar es Salaam,
Tel: +255 222 666355/57, Fax: 2668015,
Email: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania,
Website: www.sikika.or.tz

إرسال تعليق