Dodoma/Dar. Pamoja na maneno mengi yaliyosemwa, shutuma lukuki zilizotolewa na mbinu za kila aina kutaka kuzuia mjadala wa ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya IPTL, leo ndiyo siku yake ya hukumu.
Katika hukumu hiyo, ukweli utadhihirika kuhusu
nani mkweli na nani mwongo wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), itakapowasilisha bungeni maoni yake kuhusu ripoti ya kuchotwa kwa
Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Uchunguzi huo ulifanywa na Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa maelekezo ya Serikali baada ya
kuombwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alipolalamikia
ufisadi huo bungeni.
Pamoja na juhudi za kampuni ya IPTL na PAP
kufungua kesi kuzua mjadala huo bungeni, hukumu iliyotolewa jana na
majaji watatu ilisema kila kitu kiendelee kama kilivyo na
kitakachoendelea kisiathiri kesi iliyopo mahakamani.
Uamuzi huo ulipokewa kwa hisia tofauti, upande wa
IPTL ukishangilia kwa kupewa ulinzi, huku baadhi ya watu wakieleza kuwa
Mahakama imezuia mjadala huo unaosubiriwa kwa hamu.
Muda mfupi baada ya hukumu hiyo kutolewa na
kusambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, Mwenyekiti wa
PAC, Zitto Kabwe ambaye pia alikuwa mdaiwa, aliandika katika ukurasa
wake wa Twitter, “Mahakama imetoa zuio la kujadili taarifa ya CAG kuhusu
Escrow. Hata hivyo, PAC itawasilisha taarifa yake kwa mujibu wa ratiba
ya Bunge hapo kesho.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel
alisema: “Sisi hatuna taarifa hizo kutoka mahakamani, ratiba ya Bunge
inaendelea kama kawaida.”
Habari zaidi kutoka ofisi za Bunge jana, zilisema
kuwa Ofisi ya Sheria ya Bunge nayo imeshauri kuwa suala hilo linaweza
kujadiliwa bila wasiwasi wowote.
Mapema jana katika kikao cha asubuhi, Spika Anne
Makinda alilithibitishia Bunge kwamba ripoti ya escrow itajadiliwa na
hakuna wa kuwazuia.
Kauli hiyo ilitokana na mwongozo wa Mbunge wa
Bariadi (UDP), John Cheyo aliyetaka kujua kama Bunge linatambua kuwapo
kesi iliyofunguliwa mahakamani kuzuia mjadala wa ripoti hiyo.
Akijibu mwongozo huo, Makinda alisema: “Nyie
waheshimiwa wabunge msianze kuishi kwa wasiwasi, sisi kinga zetu zipo
wazi, hakuna mtu anayeweza kutushtaki sisi tusifanye kazi yetu, hayupo
atakayezuia sisi kufanya kazi za kibunge na kazi ambazo zinapatikana
kutokana na maeneo mnayopita.”
Muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa Bunge jana
usiku, Kaimu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisimama kuomba
mwongozo juu ya hatua hiyo ya Mahakama lakini Mwenyekiti wa Bunge, Mussa
Azzan Zungu alimkatisha akisema kiti cha Bunge hakijapata taarifa
zozote na kwamba msimamo uliotolewa mapema na Spika Makinda ndiyo
unaofuatwa.
- Soma Zaidi Hapa (Mwananchi)
- Soma Zaidi Hapa (Mwananchi)
إرسال تعليق