Silaha zaidi zapatikana msikitini

 
POLISI wa Kaunti ya Mombasa jana walifanya msako mwingine wa alfajiri katika misikiti miwili ya Kisauni ambako magenge yaliyokuwa na mapanga yalishambulia wakazi Jumatatu usiku.

Washukiwa 109 walikamatwa wakati wa msako huo na silaha zaidi zikapatikana.

Baada ya operesheni hiyo katika misikiti ya Swafaa na Minaa polisi walionyesha silaha mbalimbali zikiwemo gruneti, mabomu tisa ya petroli, risasi mbili, kilipuzi cha bomu, kiongeza nguvu ya bomu na mapanga matatu.

Vifaa vingine vilivyopatikana humo ni vitabu vyenye mafundisho ya Kiislamu. 
“Tulipokea habari za ujasusi kwamba misikiti kadha Kisauni inawafunza vijana siasa kali, hasa mafunzo ya jihadi.

Tulifanya operesheni kote katika kaunti hiyo ndogo tukilenga hasa misikiti iliyotajwa katika ripoti tulizopokea,” afisa mkuu wa polisi eneo la Kisauni (OCPD) Richard Ngatia akaambia wanahabari.

Katika Msikiti Minaa, polisi walimkamata mtu mmoja na kupata mapanga matatu na kisu.

Bw Ngatia alisema hakuna aliyekamatwa katika Msikiti Swafaa. “Vijana waliokuwemo walitoroka kupitia lango la nyuma na kuruka ua la ukuta”.

Katika Masjid Swafaa ambao majuzi uligonga vichwa vya habari baada ya vijana kuutwaa, polisi walisema walipata gruneti, mabomu ya petroli, kilipuzi cha bomu, kiongeza nguvu ya bomu, vifaa vinavyohusishwa na mafunzo ya jihadi na vitabu vyenye maandishi ya chuki dhidi ya vyombo vya habari.

“Ni wazi kwamba yanayoendelea ndani ya misikiti hii ni zaidi ya mahubiri na sala. Hat u t a t u l i a , tutawasaka kila kona,” akaonya Bw Ngatia.

Mkuu huyo wa polisi alisema hawakupata upinzani wowote wakati wa msako huo ulioanza saa sita usiku na kuongeza kuwa misikiti hiyo itafungwa hadi watakapokamilisha uchunguzi huku akiwataka waumini wasali katika misikiti mingine.

“Kwa sasa misikiti hiyo ni eneo la uhalifu na hakuna anayefaa kuingia humo. 
Pia tunatambua matokeo yatakayofuata na tumeweka mikakati kuhusu jinsi ya kukabiliana nayo,” akasema.

Bw Ngatia aliongeza kuwa wako tayari kukagua watu 109 waliokamatwa ili wasio na hatia miongoni mwao waachiliwe huru.

Aliwahimiza wazazi wafuatilie kwa makini mienendo ya watoto wao hasa wanakoenda kuswali.

“Fikiria sana ni wapi watoto wako wanaenda kuabudu.

Kama mzazi hufai kuruhusu watoto wako kwenda kokote kule eti kwa sababu ni mahali kwa ibada,” akasema.

Kufikia wakati tukienda mitamboni jana jioni, polisi bado hawakuwa wamekamata wanasiasa ambao Kamishna wa Kaunti Nelson Marwa alisema walifadhili magenge yaliyoua watu wanne na kujeruhi vibaya wengine saba.

W a t a t u kati yao walidungwa kisu na kuuawa katika steji tatu za basi Kisauni na wakatambuliwa kuwa Joshua Muteti, 35, Fadhili Juma Yuyu, 33, na Zephania Njeru Nyagah.

Bw Yuyu alizikwa Jumanne na maiti za wengine zikapelekwa katika hospitali kuu ya Coast General, Mombasa.

Bw Fanuel Mogesani na Bw Juma Ameena Mbere jana wanaendelea kutibiwa hospitalini humo kutokana na majeraha ambayo walipata baada ya kushambuliwa na vijana hao. 
- Taifa Leo

Post a Comment

Previous Post Next Post