TAFITI Nchini zimeonyesha kuwa kila mwaka kumekuwa na ongezeko la kesi mpya za wagonjwa kansa ya tezi dume.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORIC) umeonysha
kuwa katika mwaka 2013 idadi ya kesi mpya za waliohudhuria taasisi
hiyo ilifikia 115 kutoka 51 mwaka 2006.
Akizungumzia jana jijini Dar es Salaam, kuhusiana na uchunguzi wa hali
ya tezi dume nchini, Mwenyekiti wa Hospitali ya Apollo yenye makao
makuu nchini India, Dk. Prathap Reddy, alisema ugonjwa huo unaathiri
wanaume wengi na kusababisha vifo kwa sababu ya ukosefu wa ufahamu wa
kina juu ya ugonjwa huo.
Alisema utaratibu wa uchunguzi wa saratani ya tezi dume haufanyiki
kutokana na gharama na ukosefu wa vifaa vya uchunguzi nchini.
“Watu wengi hufika hospitalini wakati ugonjwa huo upo katika hatua ya
mwisho na hauwezi kuzuilika tena, hata hivyo, ugonjwa huo una uwezekano
mkubwa wa kutibika endapo utagundulika mapema,"alisema.
Alisema licha ya kuwepo kifaa maalum cha utambuzi wa kansa ya tezi
dume (PSA) duniani, Watanzania wachache ndio wenye uwezo wa kupata
huduma hiyo.
“Tafiti zilizofanyika hivi karibuni zinaonyesha kuwa wanaume walio chini
ya miaka 40 wana uwezekano wa kupata saratani ya tezi dume,”alisema.
Dk. Reddy, alisema kutokana na ugonjwa huo wameamua kuanzisha
kampeni ili kukusanya fedha na kutoa mwamko wa ufahamu katika masuala
ya afya kwa wanaume.
Kampeni hiyo itaitwa "masharubu" na "Novemba", ikiwa na lengo la
kuongeza ufahamu na mwamko kwa kupima ili kugundua mapema kansa,
utambuzi na matibabu ya ufanisi kwa lengo la kupunguza idadi ya vifo na
hatimaye kuzuilika kabisa,”alisema.
Alizitaja sababu zinazosababisha saratani tezi dume ni miaka, historia
ya familia, kabila, chakula, vinjwaji, uvutaji sigara, uzito, dawa na
aina ya pili kisukari.
- Tanzania Daima
Post a Comment