KAMPUNI ya uuzaji wa bidhaa za mafuta nchini, Gapco imezindua programu aminifu kuwezesha wamiliki wa magari kujipatia pointi wanunuapo mafuta ambazo zitawawezesha kupata mafuta bure kama faida.
Mpango huo utawanufaisha wakazi wa Dar es Salaam kwa kuanzia na nchini kote mwakani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo katika kituo cha Gapco Kamata Dar es Salaam jana, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, alisema kuanzishwa kwa programu ya ‘Gapco Safari’, kutasaidia kutatua changamoto za muda mrefu zinazowakabili wamiliki wa magari nchini na kwamba, mfumo huo ni muhimu kuelekea jamii ya kufanya malipo bila fedha taslimu.
Silaa, alipongeza Gapco kwa kuwa kampuni ya kwanza katika sekta ya mafuta kurudisha thamani ya fedha kwa wateja wake, na kuomba zingine kufuata nyayo hizo.
Alibainisha kuwa, huduma hiyo itasaidia kupunguza kwa ujumla gharama za mafuta, kupunguza bugudha ya makaratasi na kusaidia kuendesha biashara kwa ufanisi zaidi.
Silaa, aliongeza kwamba maendeleo kama hayo ni muhimu katika kuboresha uchumi wa nchi kwa kuwa, usafiri ni moja ya nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania na Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kuboresha sekta ya usafiri nchini.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Gapco, Dk. Macharia Irungu, alisema Gapco ina maslahi mapana katika soko la Afrika Mashariki na inajivunia kuwa na vituo vya mafuta 63 nchi nzima na kuifanya kuwa moja ya kampuni ya mafuta inayoongoza.
Aawali akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua rasmi mpango huo, Ashok Dhar, Rais wa Reliance Industries Limited India, kampuni mama ya Gapco Tanzania Ltd, alisema kuwa mpango huo unawakilisha sehemu ndogo ya faida ya Gapco.
Post a Comment