Uandikishaji serikali za mitaa waanza kwa kusua

Uandikishaji serikali za mitaa waanza kwa kusua 
JANA ikiwa ni siku ya kwanza ya uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu, Tanzania Daima imebaini mwitikio wa wananchi umekuwa mdogo katika maeneo mbalimbali.
Tanzania Daima ilitembelea vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam na kubaini vituo vingi vikiwa havina watu huku kwenye daftari la wanaojiandikisha ikionekana idadi ndogo ya watu waliojitokeza.
Baadhi ya vituo vilivyotembelewa kwa nyakati tofauti ni Kata ya Mchafukoge ambavyo ni Mchafukoge yenyewe idadi ikionyesha wamejiandikisha wapiga kura 10, Jamhuri ‘A’  saba, Jamhuri ‘B’ tisa, vyote viko Mtaa wa Kitumbini.
Joyce Ndowo ambaye ni Karani wa Kituo cha Mchafukoge, alisema idadi hiyo ndogo ilichangiwa na watu kutopata taarifa kiwango cha kutosha, huku akibainisha baadhi ya waliowauliza walieleza kupata taarifa kwenye nyumba za ibada walikokwenda kusali.
“Nina wasiwasi kuwa gari la matangazo halikupita kwenye baadhi ya maeneo kwa ajili ya kutoa taarifa hizo za uchaguzi kwamba uandikishaji wapiga kura ungeanza leo,” alisema Joyce.
Aidha, changamoto walizokumbana nazo ni watu ambao hawajafikia umri wa kupiga kura kujitokeza kwa wingi kwenye vituo hivyo wakitaka nao waandikishwe.
Naye Mtendaji wa Mtaa wa Kivule, Julius Jekura, alisema Kituo cha Kantivale waliojiandikisha ni 55, shule ya Msingi Kivule 120 na shule ya Msingi Misitu 89 vyote hivyo vikiwa katika Wilaya ya Ilala.
Diwani Kata ya Sinza Manispaa ya Kinondoni, Renatus Pamba, alisema katika Kata yake kulikuwa na vituo vinne vya uandikishaji, ambako Sinza ‘E’ iliongoza kwa waliojitokeza ambao walikuwa  270, Sinza ‘C’ 130, Sinza ‘D’ 133  na Sinza ‘B’ 80.
Naye Wakala wa Ukawa, Deus Vedasto, alisema waliojitokeza kujiandikisha katika kituo cha Mtaa wa Makangira Kata ya Msasani walikuwa 543.
Kwa upande wa Manispaa ya Temeke, Kituo cha Bustani WEO ‘A’ Kata ya Mtoni  mpaka kituo kinafungwa, Karani Joyce Fwaja alisema waliojiandikisha walikuwa 51, Kituo cha Bustani WEO ‘B’ Karani Mwanamisi Abdallah alisema walioajiandikisha ni 52, huku Bustani ‘C’ Karani Selina Dassu alisema ni 96 na Karani Francisco Sondole wa kituo cha Bustani ‘D’ alisema waliojiandikisha ni 148.
Karani Dassu, alidai kuwa wananchi hawajapewa elimu ya kutosha, hivyo idadi ya watu waliojitokeza ni chache hususani wanawake.
Jijini Tanga, nako mwamko ulikuwa wa chini huku wananchi wengi wakiendelea na shughuli zao bila kujua kama uandikishaji umeanza.
Kituo cha Magomeni A waliojiandikisha walikuwa 154, mtaa wa Fadhila 112 huku mtaa wa kanisani wakiwa 47.
Lakini baadhi ya makarani wamesema ingawa leo ni siku ya kwanza, wananchi wengi wamehamasika tofauti na walivyofikiri.
“Ingawa leo ndio kwanza siku ya kwanza hatuna hofu  na zoezi hili, tunaamini litafanikiwa kutokana na watu kuitikia,” walisema.
Patrick Mshau ni mwandishi wa daftari hilo mtaa wa kanisani, ambaye aliwataka
wananchi kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha jambo hilo muhimu.

“Tabia ya wananchi watakuja kupanga foleni ndefu siku za mwishoni, ambapo watasababisha mrundikano usio kuwa na tija, hivyo nawaomba wajitokeze mapema ili kupata haki ya kupiga kura,” alisema Mshau.
- Tanzania Daima

Post a Comment

Previous Post Next Post