CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kimetangaza
kusitisha huduma za usafiri nchi nzima keshokutwa endapo madai yao ya
msingi hayatashughulikiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(Sumatra).
Taboa ilifikia hatua hiyo katika mkutano wake mkuu uliofanyika jijini Dar es Salaam, juzi.
Kwa mujibu wa Mweka Hazina wa Taboa, Issa Nkya, mgomo huo una lengo
la kuishinikiza Sumatra isikilize kero zao ambazo zimedumu kwa muda
mrefu sasa.
“Tumekubaliana kwa kauli moja, wamiliki wa mabasi 180 tuliokutana
juzi mjini Dar es Salaam kwamba, kama Sumatra haitaki kusikiliza kero
zinazotukabili, tutasitisha huduma kwa siku mbili, yaani Jumatano na
Alhamisi.
Alisema walikuwa na kikao ambacho kiliwapa majukumu mazito yakiwamo
kuhakikisha faini ya sh 250,000 inayotozwa na Sumatra isitishwe, kwani
kubwa na inawaumiza kibiashara.
Nkya, alisema kitendo cha Sumatra kugoma kuhudhuria mkutano wao mkuu,
kinaonyesha wazi namna ambavyo haiko tayari kumaliza matatizo na
wamiliki wa mabasi.
“Juzi tulikuwa na mkutano mkuu wa chama, tukawaalika Sumatra waje
tuwaleze matatizo yetu, lakini hakuna hata kiongozi mmoja aliyekuja,
sasa unafikiri tufanye nini? dawa hapa ni kusitisha huduma tu,” alisema
Nkya.
Alisema katika mkutano huo, wamiliki wa mabasi wamelitaka jeshi la
polisi na Sumatra kuacha kufungia kampuni pindi basi moja wapo
linapopata ajali.
“Moja ya azimio letu ni kwamba, tunalitaka jeshi la polisi na Sumatra
pindi dereva anapofanya makosa iwe kuangusha basi kampuni nzima
isifungiwe, bali aadhibiwe yeye. Unakutaka kampuni moja ina mabasi 50
imeajiri wafanyakazi wengi, ukifunga kampuni hawa wote wanakwenda wapi?
lakini kubwa sisi tunatakiwa kurudisha mikopo benki kila mwezi, sasa
kwa hali hii tutafika kweli?” alihoji Nkya.
Kuhusu rushwa, Nkya alisema wanasikitishwa na trafiki wa kituo cha
Chalinze ambao wamekuwa mabingwa wa kupokea rushwa na kuandika makosa
ambayo hayana msingi.
“Jiulize basi inaondoka Ubungo baada ya kukaguliwa na trafiki vizuri,
inapita Mailimoja-Kibaha inakaguliwa tena, eti hata kama kioo kina
nyufa kidogo unaombwa fedha. Fikiria kutoka Mailimoja mpaka Chalinze
kioo kinaweza kupasuka dereva atafanyaje?” alihoji Nkya.
Katika hatua nyingine, Taboa imeitaka serikali kusitisha shughuli za
ujenzi ndani ya kituo cha mabasi Ubungo, kutokana na kukosa mwelekeo.
“Tunaitaka Serikali isitishe ujenzi ndani stendi ya Ubungo, hivi sasa
wananchi wanaokuja hapa wanateseka na vumbi, tunawataka wajenge stendi
mpya za Mbezi na Tegeta ili tuhamie huko kuliko kuendelea kuteseka
hapa,” alisema Nkya.
Wakati huo huo, mkutano mkuu wa chama hicho umewapitisha kwa kauli
moja viongozi wake kuendelea kushika nyadhifa kwa miaka tatu.
Waliopitishwa ni Mwenyekiti Mohamed Hood, Makamu Mwenyekiti Mohamed
Abdallah, Katibu Ennea Mrutu, Katibu Msaidizi Severine Ngallo, Mweka
Hazina Issa Nkya na msaidizi wake Ali Nahd.
Post a Comment