Wamiliki mabasi watangaza mgomo

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kimetangaza kusitisha huduma za usafiri nchi nzima keshokutwa endapo madai yao ya msingi hayatashughulikiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Taboa ilifikia hatua hiyo katika mkutano wake mkuu uliofanyika jijini Dar es Salaam, juzi.
Kwa mujibu wa Mweka Hazina wa Taboa, Issa Nkya, mgomo huo una lengo la kuishinikiza Sumatra isikilize kero zao ambazo zimedumu kwa muda mrefu sasa.
“Tumekubaliana kwa kauli moja, wamiliki wa mabasi 180 tuliokutana juzi mjini Dar es Salaam kwamba, kama Sumatra haitaki kusikiliza kero zinazotukabili, tutasitisha huduma kwa siku mbili, yaani Jumatano na Alhamisi.
Alisema walikuwa na kikao ambacho kiliwapa majukumu mazito yakiwamo kuhakikisha faini ya sh 250,000 inayotozwa na Sumatra isitishwe, kwani kubwa na inawaumiza kibiashara.
Nkya, alisema kitendo cha Sumatra kugoma kuhudhuria mkutano wao mkuu, kinaonyesha wazi namna ambavyo haiko tayari kumaliza matatizo na wamiliki wa mabasi.
“Juzi tulikuwa na mkutano mkuu wa chama, tukawaalika Sumatra waje tuwaleze matatizo yetu, lakini hakuna hata kiongozi mmoja aliyekuja, sasa unafikiri tufanye nini? dawa hapa ni kusitisha huduma tu,” alisema Nkya.
Alisema katika mkutano huo, wamiliki wa mabasi wamelitaka jeshi la polisi na Sumatra kuacha kufungia kampuni pindi basi moja wapo linapopata ajali.
“Moja ya azimio letu ni kwamba, tunalitaka jeshi la polisi na Sumatra pindi dereva anapofanya makosa iwe kuangusha basi kampuni nzima isifungiwe, bali aadhibiwe yeye. Unakutaka kampuni moja ina mabasi 50 imeajiri wafanyakazi wengi, ukifunga kampuni hawa wote wanakwenda wapi? lakini kubwa sisi tunatakiwa kurudisha mikopo benki kila mwezi, sasa kwa hali hii tutafika kweli?” alihoji Nkya.
Kuhusu rushwa, Nkya alisema wanasikitishwa na trafiki wa kituo cha Chalinze ambao wamekuwa mabingwa wa kupokea rushwa na kuandika makosa ambayo hayana msingi.
“Jiulize basi inaondoka Ubungo baada ya kukaguliwa na trafiki vizuri, inapita Mailimoja-Kibaha inakaguliwa tena, eti hata kama kioo kina nyufa kidogo unaombwa fedha. Fikiria kutoka Mailimoja mpaka Chalinze kioo kinaweza kupasuka dereva atafanyaje?” alihoji Nkya.
Katika hatua nyingine, Taboa imeitaka serikali kusitisha shughuli za ujenzi ndani ya kituo cha mabasi Ubungo, kutokana na kukosa mwelekeo.
“Tunaitaka Serikali isitishe ujenzi ndani stendi ya Ubungo, hivi sasa wananchi wanaokuja hapa wanateseka na vumbi, tunawataka wajenge stendi mpya za Mbezi na Tegeta ili tuhamie huko kuliko kuendelea kuteseka hapa,” alisema Nkya.
Wakati huo huo, mkutano mkuu wa chama hicho umewapitisha kwa kauli moja viongozi wake kuendelea kushika nyadhifa kwa miaka tatu.
Waliopitishwa ni Mwenyekiti Mohamed Hood, Makamu Mwenyekiti Mohamed Abdallah, Katibu Ennea Mrutu, Katibu Msaidizi Severine Ngallo, Mweka Hazina Issa Nkya na msaidizi wake Ali Nahd.

Post a Comment

أحدث أقدم