UFANYEJE MWENZI WAKO ANAPOKOSA HAMU YA TENDO?-2

Uhali gani mpenzi msomaji wa kona hii mahususi kwa ajili ya wapendanao, ni matumaini yangu kwamba uko poa na unaendelea fresh na majukumu ya kila siku. Ni wiki nyingine tunapokutana katika uwanja wetu huu, kujadili mambo mbalimbali yahusuyo sanaa ya mapenzi.
Wiki iliyopita tulianza kujadili mada hii ya mbinu za kufanya ili kumsaidia mwenzi wako aliyepoteza hamu ya tendo la ndoa. Nilichokigundua ni kwamba wengi wanasumbuliwa na tatizo hili lakini hawana pa kusemea wala hawajui wafanye nini.
NINI CHA KUFANYA?
Baada ya wiki iliyopita kuangalia jinsi tatizo la kukosa hamu ya tendo kwa mwanamke linavyotokea na dalili zake, leo tuangalie mbinu za kufanya mwenzi wako anapokuwa katika hali hii ili kumrudisha kwenye hali yake ya kawaida.

Kama nilivyosema awali, zipo sababu nyingi zinazosababisha hisia za mwanamke kuisha na kupoteza kabisa hamu ya kukutana faragha na mwenzi wake.
Tuliona jinsi migogoro ya kimapenzi, msongo wa mawazo, pilika za maisha na kushindwa kutoshelezwa kwenye tendo kunavyosababisha wanawake wengi kupoteza hamu ya kukutana na wenzi wao faragha.
Ili kukabiliana na tatizo hili, ni vizuri kuanza kushughulikia sababu zilizomfanya mwenzi wako akafikia kwenye hatua hiyo mbaya.

1. SHUGHULIKIA MIGOGORO YA KIMAPENZI
Endapo kuna tatizo limetokea kati yako na mwenzi wako, kwa mfano mwenzi wako anahisi unamsaliti kwa kutoka na mwanamke mwingine, humshirikishi kwenye mipango ya familia, hajui hata mshahara wako ni kiasi gani na unatoka lini, unaleta ubabe ndani ya nyumba, unachelewa kurudi nyumbani bila sababu, humtoi ‘out’ wala humnunulii zawadi, atahisi humpendi.

Atabaki na vinyongo na manung’uniko ndani ya moyo wake na taratibu ataanza kupoteza hisia za mapenzi juu yako. Ni lazima kila mgogoro unapotokea, ukashughulikiwa kwa busara ili kila mmoja aridhike na kuondoa dukuduku ndani ya moyo wake.
Wanawake wengi ni mahodari wa kukaa na vinyongo ndani ya mioyo yao hivyo kama mwanaume hujui namna ya kumaliza kabisa matatizo, umpendaye ataishia kwenye hali ya kupoteza hamu ya kuwa na wewe faragha. Mpe nafasi mwenzi wako azungumze hisia zake na hiyo itamsaidia kutoa vinyongo na manung’uniko.
2. MSAIDIE KUPAMBANA NA MSONGO WA MAWAZO
Njia nzuri ya kupambana na ‘stress’ zinazosababishwa na kazi, ni vizuri wanaume kuwa wanaelewa nini wenzi wao wanahitaji wanapotoka kazini. Hii inawahusu zaidi wanawake wanaofanya kazi kwani wengi wao wanaongoza kwa kupoteza hamu ya tendo kutokana na matatizo wanayokutana nayo kutwa nzima wakiwa kazini.

Zungumza kwa upole na mwenzi wako akirudi kutoka kazini, muulize jinsi siku yake ilivyokuwa, muulize mambo yaliyomkwaza kwa siku nzima na yale yaliyomfurahisha. Mpe pole kwa kazi, mtie moyo pale alipokosea na mfanye ayaone matatizo ya kazini kuwa sehemu ndogo ya maisha yake.
Hiyo itamfanya ajihisi kuwa kwenye mikono salama na atasahau kero zote alizokutana nazo kutwa nzima, hata mkipanda kitandani, atakuwa mtu mpya na atafurahia kuwa na wewe faragha. Kama kazi anazofanya zinahusisha mwili kuchoka, si vibaya kama ukamfanyia mkeo ‘masaji’ ya kupunguza uchovu.
Wengi wanaamini kwamba wanaume ndiyo watu wa kufanyiwa vitu hivyo tu, la hasha, hata wanawake nao kuna muda wanahitaji ili kurudi kwenye utulivu wa kihisia.

Itaendelea wiki ijayo.

Post a Comment

أحدث أقدم