Ukawa kunufaika mgogoro wa madiwani Bukoba

Bukoba.  Athari za mgogoro wa kisiasa katika Manispaa ya Bukoba huenda zikaanza kuonekana katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14, mwaka huu baada ya vyama vya upinzani kugawana maeneo ili kutumia mpasuko ndani ya CCM kushinda viti vingi.
Vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF katika Manispaa ya Bukoba ambavyo kitaifa vimeunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), tayari vimeafikiana kusimamisha mgombea mmoja kila mtaa kwa kuzingatia nguvu ya chama katika mtaa husika.
Manispaa ya Bukoba ina jumla ya mitaa 66 na kwa mujibu wa katibu wa CUF katika Manispaa ya Bukoba, Ramadhani Bahati chama hicho kimesimamisha wagombea katika mitaa 20 na maeneo mengine kuachia vyama rafiki.
Katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa, Chadema na CUF zilishinda mitaa minne katika manispaa hiyo, vikigawana miwili kila kimoja na kuiachia CCM mitaa 62.
“Kuna mgogoro mkubwa kati ya (Balozi Khamisi) Kagasheki na (Anatory) Dk Amani uliokigawa chama chao. Tumetumia mpasuko wao kusimamisha wagombea wachache ambao tuna uhakika watashinda, hiyo ni fursa kubwa kisiasa kwetu,” alisema Bahati.
Kagasheki ni mbunge wa Bukoba Mjini na Dk Amani ni meya wa Manispaa ya Bukoba.
Pia alisema Chadema na NCCR Mageuzi zimesimamisha wagombea kwa kuzingatia utaratibu huo wa kugawana mitaa 46 na kwamba kutokana na mpasuko uliopo ndani ya CCM, hawana wasiwasi wa ushindi.
Wakati maeneo mengine yametajwa kuongezewa mitaa kutokana na wingi wa watu, katika Manispaa ya Bukoba hakuna mtaa ulioongezeka kwa kuwa taratibu za kufikia hatua hiyo hujadiliwa pia kwenye vikao vya Baraza la Madiwani ambavyo vimesimama.
Kwa upande mwingine, tishio kubwa la CCM katika uchaguzi huo ni baadhi ya kata zilizokuwa na madiwani kuvuliwa nyadhifa hizo na mahakama, akiwamo mwenyekiti wa chama hicho wa Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza aliyekuwa diwani wa Kata ya Kashai.
Vilevile, mwenyekiti wa vijana wa CCM wa Manispaa ya Bukoba, Chifu Karumuna ambaye pia ni diwani wa Kata ya Kahororo, anahusishwa na upande mmoja kwenye mgogoro kati ya makundi hayo, hali inayopunguza hamasa ya vijana kutetea wagombea wa chama hicho katika mitaa waliyogombea.
Kutokana na mgogoro uliopo, wafuasi wa kundi la Balozi Kagasheki ni nadra kujihusisha na masuala ya chama katika maeneo ambayo kuna viongozi wanaoaminika kumuunga mkono Dk Aman, mazingira yanayowaweka wagombea wa chama hicho njiapanda dhidi ya wale wa upinzani.
Athari za makundi pia zilionekana wakati wa kumuaga aliyekuwa katibu wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Averin Mushi aliyehamishiwa Katavi ambaye alituhumiwa kumuunga mkono Dk Aman. Katika sherehe ya kumuaga, viongozi wote wa CCM wa wilaya zote walishiriki isipokuwa Manispaa ya Bukoba. - Soma zaidi Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post