
Vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF katika
Manispaa ya Bukoba ambavyo kitaifa vimeunda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), tayari vimeafikiana kusimamisha mgombea mmoja kila mtaa kwa
kuzingatia nguvu ya chama katika mtaa husika.
Manispaa ya Bukoba ina jumla ya mitaa 66 na kwa
mujibu wa katibu wa CUF katika Manispaa ya Bukoba, Ramadhani Bahati
chama hicho kimesimamisha wagombea katika mitaa 20 na maeneo mengine
kuachia vyama rafiki.
Katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa,
Chadema na CUF zilishinda mitaa minne katika manispaa hiyo, vikigawana
miwili kila kimoja na kuiachia CCM mitaa 62.
“Kuna mgogoro mkubwa kati ya (Balozi Khamisi)
Kagasheki na (Anatory) Dk Amani uliokigawa chama chao. Tumetumia mpasuko
wao kusimamisha wagombea wachache ambao tuna uhakika watashinda, hiyo
ni fursa kubwa kisiasa kwetu,” alisema Bahati.
Kagasheki ni mbunge wa Bukoba Mjini na Dk Amani ni meya wa Manispaa ya Bukoba.
Pia alisema Chadema na NCCR Mageuzi zimesimamisha
wagombea kwa kuzingatia utaratibu huo wa kugawana mitaa 46 na kwamba
kutokana na mpasuko uliopo ndani ya CCM, hawana wasiwasi wa ushindi.
Wakati maeneo mengine yametajwa kuongezewa mitaa
kutokana na wingi wa watu, katika Manispaa ya Bukoba hakuna mtaa
ulioongezeka kwa kuwa taratibu za kufikia hatua hiyo hujadiliwa pia
kwenye vikao vya Baraza la Madiwani ambavyo vimesimama.
Kwa upande mwingine, tishio kubwa la CCM katika
uchaguzi huo ni baadhi ya kata zilizokuwa na madiwani kuvuliwa nyadhifa
hizo na mahakama, akiwamo mwenyekiti wa chama hicho wa Wilaya ya Bukoba,
Yusuph Ngaiza aliyekuwa diwani wa Kata ya Kashai.
Vilevile, mwenyekiti wa vijana wa CCM wa Manispaa
ya Bukoba, Chifu Karumuna ambaye pia ni diwani wa Kata ya Kahororo,
anahusishwa na upande mmoja kwenye mgogoro kati ya makundi hayo, hali
inayopunguza hamasa ya vijana kutetea wagombea wa chama hicho katika
mitaa waliyogombea.
Kutokana na mgogoro uliopo, wafuasi wa kundi la
Balozi Kagasheki ni nadra kujihusisha na masuala ya chama katika maeneo
ambayo kuna viongozi wanaoaminika kumuunga mkono Dk Aman, mazingira
yanayowaweka wagombea wa chama hicho njiapanda dhidi ya wale wa
upinzani.
Athari za makundi pia zilionekana wakati wa
kumuaga aliyekuwa katibu wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Averin Mushi
aliyehamishiwa Katavi ambaye alituhumiwa kumuunga mkono Dk Aman. Katika
sherehe ya kumuaga, viongozi wote wa CCM wa wilaya zote walishiriki
isipokuwa Manispaa ya Bukoba. - Soma zaidi Mwananchi
إرسال تعليق