
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema
jana kwamba moja ya mikakati hiyo ni madai ya kuwapo barua ya Mahakama
kuzuia mjadala huo akisema mkakati huo unatokana na ukubwa wa kashfa na
jinsi inavyowahusisha viongozi waandamizi serikalini.
Mbatia aliyeambatana na kundi kubwa la wabunge
kutoka Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, alisema: “Iko mikakati na mbinu za
kila aina kulihujumu Bunge lisisimamie fedha za walipakodi, ndiyo maana
kuna danadana na tuna taarifa za kuwapo barua kutoka mahakamani kuzuia
jambo hilo lisijadiliwe bungeni kwa madai eti kuna kesi.
“Mahakama haiwezi kuingilia shughuli za Bunge,
inatia wasiwasi kwa kuwa Ofisi ya Bunge nayo imekuwa na danadana kila
siku kwa kubadilisha badilisha ratiba wakati sisi tunataka hawa
waliohusika kwenye kashfa hii wachukuliwe hatua.”
Pia, alisema kuna taarifa kwamba Serikali inadai haina fedha, ikitaka kufupisha Bunge na suala hilo lisijadiliwe sasa hivi.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Mnyaa
alisema: “Serikali inategesha tegesha tu mambo bungeni na ndiyo maana
leo (jana) wameahirisha Bunge hadi kesho (leo) bila sababu za msingi,
wanafinya muda wa sisi kujadili sakata hili,” alisema Mnyaa.
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu
alisema escrow ni kama ilivyokuwa kashfa ya Richmond ambayo iliwang’oa
wahusika wakuu bungeni, hivyo haiwezekani isijadiliwe bungeni kwa madai
kwamba Mahakama imezuia...
“Hakuna utaratibu kama huo wa Mahakama kuelekeza Bunge kitu gani kifanyike na gani kisifanyike pia hata Katiba hairuhusu hilo.”
Lissu alishangazwa na Naibu Spika, Job Ndugai
kuahirisha Bunge jana hadi leo kwa madai kuwa yeye (Lissu) alikuwa
hajakamilisha taarifa ya upinzani kwenye muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014 akidai kuwa huo ni
upotezaji wa muda.
“Nilimwomba Naibu Spika kuwa aahirishe muswada huo
hadi kesho kwa kuwa ulikuwa umepangwa tarehe 25 lakini ghafla
ukabadilishwa na mimi sikuwapo kwa muda wote huo. Sikuomba aahirishe
Bunge nilimwomba aahirishe muswada tu,” alisema Lissu.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema naye
amesikia kuwapo barua ya Mahakama kuzuia mjadala huo na kusema kama ni
kweli, halitakuwa sahihi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika
Operesheni Delete CCM mjini Dodoma jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa alisema si Waziri Mkuu wala Jaji Mkuu anayeweza kuuzima
mjadala wa escrow bungeni.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment