Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova amesema ulinzi utaimarishwa
kabla, wakati na baada ya mdahalo maalumu wa Katiba ulioandaliwa na
Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es
Salaam mzungumzaji mkuu akiwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Hatua ya Kova imekuja baada ya kuibuka kwa vurugu
zilizosababisha kuvunjika mdahalo wa kwanza uliofanyika Novemba 2,
kwenye Hoteli ya Blue Pearl Ubungo, Dar es Salaam.
Kova alisema polisi imejiandaa kwa ulinzi ili
kudhibiti vurugu zozote zitakazotokea pamoja na kuhakikisha usalama wa
washiriki na eneo zima kwa ujumla.
“Mdahalo ule wa kwanza uliovurugwa, hatukuwa na
taarifa nao, lakini huu waandaaji wametupa taarifa hivyo tumejiandaa
kuimarisha ulinzi, ili kuhakikisha amani inatawala katika eneo hilo,”
alisema.
Juzi, Mwenyekiti wa MNF, Joseph Butiku alisema
ofisi yake inaamini kwamba mdahalo huo wa wazi kwa ajili ya Watanzania
wenye mapenzi mema utakuwa wa amani. Alisema uhakika wa usalama katika
mdahalo huo unatokana na kwamba wameshatoa taarifa kwa vyombo vya
usalama.
Alisema mdahalo wa leo ni sehemu tu ya ushiriki wa
mijadala ya umma kuhusu Katiba Inayopendekezwa, ambayo kwa sasa
inaendelea katika maeneo yote ya nchi, ikifanywa na viongozi wa kisiasa,
mashirika ya kijamii na hata watu binafsi katika vyombo mbalimbali vya
habari.
Alisema japokuwa kwa sasa wamepata ukumbi mdogo
unaoweza kuingiza watu 350, watatoa fursa kwa watu kuuliza maswali na
kupata majibu kuhusu vifungu na vipengele mbalimbali vyenye utata
vinavyoyahusu makundi yote ya kijamii ambayo yamepata uwakilishi katika
mapendekezo hayo ya Katiba
إرسال تعليق