Dar es Salaam. Maisha ya maelfu ya Watanzania yapo hatarini baada ya kubainika kuwa kwenye magari ya abiria maarufu daladala ya jijini humo, yanayotoa huduma za usiku kwa safari za kwenda na kutoka maeneo mbalimbali yamekuwa yakihusishwa na mtandao wa vibaka unaoendesha vitendo vya uporaji na ukabaji.
Mtandao huo unaelezwa kufanya vitendo hivyo kwa
kutumia silaha mbalimbali ikiwamo visu na bastola, huku baadhi ya vibaka
hao wakitumia magari hayo kujificha kwa kujifanya ni abiria.
Mbali na uhalifu huo unaoendelea kufanyika kwenye
daladala nyakati hizo za usiku, magari mengi yanayotoa huduma za usafiri
nyakati hizo hadi alfajiri ni mabovu yakiwa pia hayana vibali vya kutoa
huduma hizo.
Magari hayo yanayofahamika kwa jina la ‘daladala
bubu’ au ‘ya kuwanga’ madereva wake pia hufanya kazi hiyo bila ya kuwa
na leseni za udereva, jambo linalohatarisha zaidi maisha ya abiria.
Uchunguzi wa gazeti hili katika maeneo mbalimbali
ya jiji hilo ikiwamo Sinza, Ubungo, Kariakoo, Faya, Buguruni, Gongo la
Mboto Machinjioni, Kimara, Mbezi, Magomeni, Kinondoni, Tandika, Temeke,
Yombo Dovya, Vingunguti, Bom Bom na Machimbo, umebaini kuwa magari hayo
hufanya kazi nyakati za usiku pekee kutokana na kutokuwapo askari ama
kuwapo askari wachache wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Gazeti hili limebaini kuwa wizi kwenye daladala
hizo, madereva wa daladala kuwapa makondakta au wapiga debe kuendesha
magari ya abiria vinaendelea kushamiri, huku nyakati za hatari zaidi kwa
daladala hizo ni kuanzia saa 6 usiku hadi alfajiri.
Uhalifu unaofanywa
Uhalifu unaofanywa kwenye magari hayo unahusisha vibaka wanaokuwa ndani ya gari ambao hujifanya kuwa miongoni mwa abiria.
Imebainika kuwa abiria akikaa vibaya ndani ya
daladala, vibaka hao hutumia nafasi hiyo na kujihalalishia chochote
watakachoweza kuibia.
Aina nyingine ya vibaka ni wale wanaokula njama na
madereva na kondakta wa daladala. Vibaka hao pia hujifanya abiria
kwenye daladala bubu husika ambapo wakifika kituoni hujihusisha na
kupiga debe kuita abiria, lakini mbele ya safari dereva hubadili njia,
akiweza kwenda vichochoroni ndipo abiria huvamiwa na kuporwa mali zao
huku wakitishiwa kwa silaha.
Uchunguzi unaonyesha kuwa aina nyingine ya wizi
huo hufanywa na kundi la vibaka ambalo hujifanya ni abiria ambapo kila
mmoja hulenga kumfanyia uhalifu abiria mmoja.
“Abiria akishuka tu na yeye anashuka, humfuata na
kumwibia, halafu anakwambia utembee bila kugeuka. Ukigeuka tu
wanakuchoma na kisu au silaha yoyote wanayokuwa wamejihami nayo,”
alieleza mmoja wa madereva wa daladala aliyeomba jina lihifadhiwe kwa
kuwaogopa vibaka hao.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment