Hoja zawaumiza CCM, Makonda aongoza vijana kumshambulia
Mdahalo wavunjika, polisi waonyesha udhaifu
Meseji za kupanga vurugu zanaswa, wanavyuo wahusishwa
HOJA mbalimbali za aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba, jana ziliwafanya baadhi ya makada wa CCM kupandwa
na jazba na kuzua vurugu kubwa katika mdahalo ulioitishwa na Taasisi ya
Mwalimu Nyerere kujadili masuala yaliyomo katika Katiba iliyopendekezwa.

Mdahalo huo ambao ulipangwa kuhutubiwa na baadhi ya wajumbe wa iliyokuwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilibidi uvunjike kutokana na vurugu hizo
kubwa.
Mbali na kuvunjika kwa mdahalo huo, pia Jaji Warioba ambaye pia ni
Makamu wa Rais mstaafu katika serikali ya awamu ya Pili, alishambuliwa
kwa kupigwa na Katibu wa Uhamasishaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul
Makonda, pamoja na wafuasi wengine wa chama hicho.
Kabla ya kuanza kwa vurugu hizo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu
Nyerere, Joseph Butiku, aliwaeleza wananchi waliohudhuria mdahalo huo
dhamira yake ni kupata ufahamu wa masuala yaliyomo katika katiba na yale
yaliyoondolewa, pia kufikia uamuzi sahihi siku ya kupiga kura ya
kukataa au kukubali katiba hiyo.
Mara baada ya Butiku kumaliza kuongea, alimkaribisha mtoa mada Jaji
Warioba, ambaye alizungumzia masuala mbalimbali yaliyoboreshwa na
kuondolewa.
Muda wote Warioba alipokuwa akizungumza, wananchi walikuwa
wakimshangilia kwa makofi huku baadhi ya vijana waliopangwa kufanya
vurugu wakiwa wanahimizana kuonyesha mabango yao waliyoyaandaa juu.
Vurugu zilivyoanza
Vurugu mdahalo wavunjikaWakati Jaji Warioba akizungumzia masuala
mbalimbali, alilalamikia kitendo cha watu kumtumia Mwalimu Nyerere kama
kinga ya kufanikisha masuala yao, huku akieleza kuwa kiongozi huyo mpaka
anafariki dunia alikuwa akiamini katika azimio la Arusha.


“Laiti kama Nyerere angekuwepo asingekubali viongozi kuweka fedha nje ya
nchi, kama Nyerere angekuwepo asingekubali viongozi kupewa zawadi na
kuzificha majumbani mwao na kama Mwalimu Nyerere angekuwepo katika zama
hizi…asingeruhusu maadili ya viongozi kukataliwa kuingizwa katika
katiba,” alisema Jaji Warioba.
Kauli hiyo, iliamsha hisia za vijana waliokuwa upande wa kulia kwa Jaji
Warioba wakiongozwa na Paul Makonda, ambao waliinua mabango juu, baadhi
yakisomeka; Katiba iliyopendekezwa tumeipokea, tumeielewa, tumeikubali
na tutaipitisha.
Mengine yaliandikwa; Fedha za magharibi haziwezi kubomoa nchi yetu,
Katiba iliyopendekezwa tumeielewa na tunaiunga mkono. Kisha kuanza
kushangilia na kuimba CCM…CCM…CCM.
Baada ya hali hiyo, watu walianza kushikana mashati na viti kuanza
kurushwa ukumbini na baadhi ya watu, huku Makonda akimkimbilia Amon
Mpanju, ambaye alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kundi la
Walemavu, kumfanya kuwa kinga yake kwa kujificha mgongoni mwake.
Muda wote huo, wajumbe waliokuwa wamepangwa kutoa mada katika mdahalo
huo walikuwa wamekaa meza kuu huku baadhi ya vijana wakiwa wamewawekea
ulinzi.
Wakati viti vikiendelea kurushwa ukumbini humo na wengine kushambuliana
kwa makonde, mlinzi wa Jaji Warioba alimuondoa kiongozi huyo aliyepewa
ulinzi wa ziada na baadhi ya vijana.
Hata hivyo, Makonda alitumia nafasi hiyo kujipenyeza na kisha kumrushia
kibao cha mgongoni Jaji Warioba na vijana wengine waliokuwa karibu yake
wakaamua kumshambulia kiongozi huyo.
Katika hali hiyo, mlinzi wa Jaji Warioba alijitahidi kuzuia mikono ya
washambulizi na kisha kumbeba juu kwa juu kiongozi huyo na kumpeleka
katika chumba cha watu maalum kwa ajili ya usalama.
Kitendo hicho cha Makonda kumshambulia Jaji Warioba, kiliamsha hasira za
wananchi na kuanza kumshambulia huku kiongozi huyo wa uhamasishaji wa
UVCCM akijitahidi kukimbilia katika moja ya vyumba vya wafanyabiashara
hotelini humo kwa ajili ya kujiokoa.
Udhaifu wa kiulinzi
Muda wote wakati vurugu hizo zikiwa zinaendelea hadi Jaji Warioba
kuwekewa ulinzi na baadhi ya vijana, hakukuwa na askari yeyote na hali
ilipoanza kutulia ndipo magari mawili ya askari yakawa yamefika eneo
hilo la Ubungo Plaza na kuanza kufyatua risasi nje ya jengo hilo.
Magari ya Polisi yaliongezeka kadiri muda ulivyokuwa ukienda huku askari
wakiimarisha ulinzi na kuwazuia baadhi ya waandishi wa habari wasiweze
kupata habari ipasavyo.
Baada ya dakika 48 kupita tokea kuanza kwa vurugu hizo, baadhi ya
viongozi wa mdahalo, waliwaelekeza wananchi warudi katika viti vyao huku
wakiwaambia mdahalo utaendelea.
Mmoja wa washereheshaji wa mkutano huo, Saed Kubenea, aliwaeleza
wahudhuriaji wa mdahalo kuwa, viongozi wote wako salama na kwamba
watakaporejea eneo hilo wawahakikishie ulinzi jambo lililoshangiliwa kwa
nguvu.
Nje ya ukumbi, askari waliofika waliimarisha ulinzi katika maeneo
mbalimbali huku Butiku na wajumbe wengine kasoro Jaji Warioba, walipata
nafasi ya kurejea ukumbini na kueleza kuwa tukio lililotokea ni la aibu
kwa Taifa na kwamba, walioandaa mipango hiyo wanajulikana na
watawashughulikia.
“Walioandaa vurugu hizi tunawatambua, tutawashughulikia na kwa sababu ya hali hii tunaahirisha mdahalo,” alisema Butiku.
Warioba atolewa chini ya ulinzi mkali
Warioba atolewa chini ya ulinzi mkaliBaada ya kauli ya kuahirisha
mdahalo, askari waliongezeka nje ya chumba alichokuwa Jaji Warioba na
kuwataka wananchi kutawanyika.

Mbali na wananchi, pia waaandishi walitakiwa waondoke huku wakiambiwa Jaji Warioba hawezi kuzungumza nao kwa siku hiyo ya jana.
Wakati Jaji Warioba akiwa anatoka, watu waliokuwa nje wakimsubiri
walianza kumshangilia na baadhi wakiimba Rais…Rais…Rais, hali
iliyowafanya askari wawakamate vijana wawili waliokuwa wanashangilia na
kuwafunga pingu kisha wakawapakiza katika magari yao.
Mpango wa kuvuruga mdahalo
Habari zilizopatikana kwa baadhi ya vijana ndani ya ukumbi wa mdahalo,
zinaeleza kuwa waliofanya vurugu waliahidiwa kulipwa fedha baada ya kazi
hiyo na kwamba, mkakati huo ulifanywa siku moja kabla ukiwahusisha
baadhi ya wanavyuo.
Baadhi ya wanafunzi waliohusika wanatoka vyuo vya Mwalimu Nyerere Kigamboni na Chuo cha Usimamizi wa Maji na Maendeleo.
Baadhi ya wanafunzi hao walitumiwa ujumbe wa kwenda kufanya vurugu na
mtu mwenye namba za simu 0656 501317 aliyejisajili kwa jina la Valence
Kisima.
Katika ujumbe wake, Kisima aliwaandikia aliokusudia wakafanye vurugu
kwamba; “Kesho Jumapili kuna kongamano Ubungo Plaza, mda (Muda) ni saa
sita, nauli ipo kwa mshiriki mpe taarifa na mwenzio.
Ujumbe mwingine wa Kisima ulieleza; “But asivae rangi ya chama kijani
wala njano coz 2kio ili ni maalum sana ntawapa maelekezo kesho saa tano
nikija ukumbini.
Waliyosema awali
Awali kabla ya vurugu kuanza, Warioba alisema Watanzania hawapaswi
kujivunia takwimu ya aslimia 81 ya masuala yaliyoingizwa katika katiba
iliyopendekezwa, kwa kile alichoeleza masuala muhimu yaliyokuwa na
nafasi ya kuleta mabadiliko yamewekwa pembeni.
Alisema mengi ya mambo yaliyoingizwa katika katiba hiyo ni yale mazuri
yaliyochukuliwa katika katiba ya sasa huku masuala ya msingi
yaliyopendekezwa na wananchi yakiwa yameachwa kando.
Aliongeza moja ya jukumu la tume aliyokuwa akiiongoza ni pamoja na
kuchukua mazuri ya katiba inayotumika sasa na maoni mengine ya wananchi,
huku akisema masuala ya tunu za taifa zilizoachwa na bunge maalum ni
muhimu kwa ajili ya mabadiliko.
Butiku, alisema watazunguka katika mikoa ya Mwanza Mbeya na nchi ya
Zanzibar, kwa ajili ya kufanya midahalo kama iliyofanyika katika maeneo
mengine chini.
Alisema mdahalo wa jana, unapaswa kutafsiriwa kuwa ni wa watanzania na si wa makundi kama ilivyokuwa awali.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kujua kilichomo ndani ya katiba hiyo,
japo bado haijasambazwa kwa kiasi kikubwa na kwamba, kwa sasa inapaswa
kujadiliwa na wananchi na siyo makundi.
“Tunataka mtaani katiba hii ijadiliwe pasipo kumuogopa mtu, hakuna
kusimamiwa na yeyote wala chama chochote, katiba hii ni yenu ili kesho
na kesho kutwa usije kumlaumu mtu au kulaumiwa na mjukuu wako kwa uamuzi
mtakaofikia baada ya kura ya maoni,” alisema Butiku.
Humphrey Pole pole, aliwaeleza wahudhuriaji kuwa katiba iliyopendekezwa
inapaswa kuangaliwa kwa umakini na kwamba, wananchi kuipigia kura ya
hapana siyo dhambi.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment