Unaposikia au kuona maziwa ya mtindi, hisia zinazokufikia haraka ni zile za uchachu na ladha nzuri ya kinywaji hicho.
Lakini utafiti mpya umethibitisha kuwa mtindi ni
zaidi ya kinywaji, ni tiba ambayo inakuokoa na maradhi yasababishwayo na
mazingira yetu.
Utafiti uliofanywa nchini na Taasisi ya
Microbiology ya Marekani na kuchapishwa katika jarida la The Science
Daily umeeleza kuwa maziwa ya mtindi yana bakteria rafiki ambao wana
uwezo wa kuwalinda watoto na wajawazito na kemikali nzito za sumu.
Madaktari wa Kitanzania kwa kushirikiana na wale
wa Canada walitengeneza maziwa ya mtindi yenye bakteria hao aina ya
Lactobaciluus Rhamnosus kisha kuyagawa kwa wahusika ili kupata matokeo.
Wakiongozwa na Dk Gregor Reid, watafiti hao
walibaini kuwa bakteria hao wana uwezo wa kumkinga mtu na mazingira
yanayohatarisha afya katika maeneo duni duniani.
“Tulibaini kuwa metali na kemikali zenye sumu
zinazuiwa kuingia kwenye mwili wa binadamu hasa wakati wa kula iwapo mtu
atatumia maziwa ya mtindi,” ilisema sehemu ya utafiti huo.
Akifanya kazi na Taasisi ya Western Heads East, Dk
Reid ameanzisha mpango wa kutengeneza bakteria hao katika baadhi ya
jamii mkoani Mwanza.
Nia ni kuanza kuusaidia mkoa huo ambao upo katika
Ziwa Victoria ambalo limeathiriwa kwa kiasi kikubwa na dawa za kuua
wadudu na sumu nyingine za metali pamoja na zebaki.
Akielezea manufaa ya maziwa ya mtindi kwa afya,
Mtaalamu wa Chakula na Lishe kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Pazi
Mwinyimvua anasema kuwa, uchakataji wa mtindi huendana na bakteria
wazuri ambao ni kinga tosha mwilini ya baadhi ya magonjwa.
Mwinyimvua anabainisha kuwa uchachu uliopo
unatokana na vunjavunja ya maziwa na kupatikana mtindi ambapo hali hiyo
ndiyo huleta faida nyingi.
“Kwa mfano unapokula chungwa moja unapata faida
ndogo tofauti na unapokunywa bilauri moja ya juisi yake kwa kuwa inakuwa
imeshasagwa na kuchujwa, ni sawa na mtindi ule utaratibu wa kuhama
kutoka katika maziwa ya kawaida na kuwa mtindi, ndiyo unaoongeza
vitamini na faida ya kujikinga na maradhi mbalimbali,” anasema Pazi.
Dk Badru Mustapha anavitaja virutubisho
vinavyopatikana kwenye mtindi kuwa ni pamoja na ‘Calcium’, ‘Phosphorus’,
‘Riboflavin (vitamin B2), ‘Iodine’, ‘vitamin B12’, ‘Pantothenic acid
(vitamin B5) ‘Zinc’, ‘Potassium’ na ‘Molybdenum’ ambavyo ni kinga tosha
mwilini.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق