Utafiti Polisi Jamii waonyesha mafanikio

Utafiti Polisi Jamii waonyesha mafanikioJESHI la Polisi nchini limetakiwa kutumia matokeo ya utafiti wa tathmini ya Polisi Jamii uliofadhiliwa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kuboresha mkakati wa Polisi jamii ili kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Utafiti huo ulifanywa kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambako imeelezwa una manufaa makubwa katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu na kero mbalimbali katika jamii.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Selina Lyimo, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, wakati wa hafla ya kukabidhi chapisho la utafiti wa matokeo ya tathmini ya Polisi jamii nchini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbaraka Abdulwakili .
Kwa upande wake, Abdulwakili alisema atahakikisha utafiti huo unafanyiwa kazi ipasavyo na kuwataka watendaji wa Jeshi la Polisi kuutumia katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao, kwa kuwa askari waliopo hawatoshi na Polisi Jamii imeonyesha  mafanikio makubwa katika kuzuia vitendo vya uhalifu na wahalifu.
Naye, Mtaalamu Mwelekezi wa Utafiti wa Tathmini ya Polisi Jamii ambaye pia ndiye Mtafiti Mkuu, Dk. Haji Semboja, alisema kuwa utafiti huo ulifanyika katika kanda saba, ambako matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa uhusiano wa kiutendaji baina ya wananchi na Jeshi la Polisi umeboreshwa kupitia dhana ya Polisi Jamii.
Alisema kuwa, jambo hilo linasaidia katika kutengeneza mazingira ya amani na hivyo shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii zinaweza kuendelea kufanyika bila hofu na kwa uhakika wa ulinzi na usalama.
Naye Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki, aliipongeza timu nzima iliyofanya utafiti huo na kwamba, Jeshi la Polisi kama watekelezaji wakuu wa programu ya maboresho  yaliyojikita katika mihimili mikuu mitatu ambayo ni weledi, usasa na Polisi Jamii.
Alisema wanatambua na kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na watafiti hao na kuwaomba kuangalia namna wanavyoweza kufanya utafiti katika mihimili mingine miwili iliyobaki ambayo ni usasa na weledi ili Jeshi liweze kuwa na tathimini halisi ya maboresho yake.
- Tanzania Daima

Post a Comment

Previous Post Next Post