JESHI
la Polisi nchini limetakiwa kutumia matokeo ya utafiti wa tathmini ya
Polisi Jamii uliofadhiliwa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia kuboresha mkakati wa Polisi jamii ili kuimarisha ulinzi na
usalama wa raia na mali zao.
Utafiti huo ulifanywa kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH), ambako imeelezwa una manufaa makubwa katika kubaini, kuzuia
na kutanzua uhalifu na kero mbalimbali katika jamii.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Selina
Lyimo, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, wakati wa hafla ya kukabidhi chapisho la utafiti wa matokeo
ya tathmini ya Polisi jamii nchini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mbaraka Abdulwakili .
Kwa upande wake, Abdulwakili alisema atahakikisha utafiti huo
unafanyiwa kazi ipasavyo na kuwataka watendaji wa Jeshi la Polisi
kuutumia katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao, kwa kuwa askari
waliopo hawatoshi na Polisi Jamii imeonyesha mafanikio makubwa katika
kuzuia vitendo vya uhalifu na wahalifu.
Naye, Mtaalamu Mwelekezi wa Utafiti wa Tathmini ya Polisi Jamii
ambaye pia ndiye Mtafiti Mkuu, Dk. Haji Semboja, alisema kuwa utafiti
huo ulifanyika katika kanda saba, ambako matokeo ya utafiti huo
yanaonesha kuwa uhusiano wa kiutendaji baina ya wananchi na Jeshi la
Polisi umeboreshwa kupitia dhana ya Polisi Jamii.
Alisema kuwa, jambo hilo linasaidia katika kutengeneza mazingira ya
amani na hivyo shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii zinaweza
kuendelea kufanyika bila hofu na kwa uhakika wa ulinzi na usalama.
Naye Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki,
aliipongeza timu nzima iliyofanya utafiti huo na kwamba, Jeshi la Polisi
kama watekelezaji wakuu wa programu ya maboresho yaliyojikita katika
mihimili mikuu mitatu ambayo ni weledi, usasa na Polisi Jamii.
Alisema wanatambua na kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na watafiti
hao na kuwaomba kuangalia namna wanavyoweza kufanya utafiti katika
mihimili mingine miwili iliyobaki ambayo ni usasa na weledi ili Jeshi
liweze kuwa na tathimini halisi ya maboresho yake.
- Tanzania Daima
إرسال تعليق