Dar es Salaam. Hatima ya kashfa ya kudanganya
umri inayomkabili aliyekuwa mrembo wa Tanzania mwaka 2014, Sitti Mtemvu
bado ipo kizani baada ya polisi kuikana kauli ya Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (Rita).
Rita, kwa upande wao ilieleza wiki moja iliyopita
kuwa imekabidhi polisi vielelezo kuhusu uchunguzi wa kashfa hiyo kwa
lengo la kuchukua hatua.
Jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova alikana kupokea taarifa za vielelezo hivyo
vilivyotumiwa kuombea cheti cha kuzaliwa cha Sitti Mtemvu.
Wiki mbili zilizopita, Wizara ya Habari,
Utamaduni, Vijana na Michezo kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata)
ilijivua lawama katika kashfa hiyo na kuiachia Rita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kova alisema,
“Jeshi la Polisi halijapokea vielelezo vyovyote kutoka Rita, wamepeleka
wapi? Iwapo waliviwasilisha katika kituo chochote cha polisi watoe
taarifa iliyo sahihi, iwapo vielelezo hivyo vitatufikia tutachukua hatua
stahiki,” alisema Kova.
Kwa upande wao, Rita waliahidi kuwasilisha
vielelezo hivyo wiki hii na kwamba vilicheleweshwa kutokana na
kukamilisha upekuzi wa taarifa za kuombea cheti pamoja na cheti cha
awali kilichokuwa kikitumiwa na Sitti Mtemvu.
Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Rita, Emmy
Harrison alisema jana kuwa idara yake imekamilisha taratibu zote
zinazotakiwa na vielelezo hivyo vitakabidhiwa rasmi polisi.
“Haya ni masuala ya kisheria, hivyo sisi
tumeshakamilisha kile tulichotakiwa kukifanya na mchakato huu bado
unaendelea, tupo katika maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kuripoti
polisi, wiki hii vielelezo vya Sitti vitapelekwa kwenye vyombo vya
usalama kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema Harrison.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق