Utulivu utawale mjadala wa Akaunti ya Escrow

Baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuwasilisha bungeni ripoti kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow juzi, tunapenda kulipongeza Bunge kwa kuipa kamati hiyo ya PAC, chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe jukumu la kuchunguza na kupata ukweli kuhusu Sh306 bilioni zinazodaiwa kuchotwa katika mazingira ya kutatanisha kutoka kwenye akaunti hiyo iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Tunaipongeza pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa kuiwezesha PAC kupata taarifa muhimu katika kukusanya na kuandika ripoti iliyoiwasilisha bungeni.
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), nayo inastahili pongezi kwa kuandaa na kutoa taarifa za kina kwa PAC kuhusu Akaunti hiyo ya Tegete Escrow.
Kama wengi wanavyofahamu, ofisi hiyo ya CAG, kwa muda mrefu sasa imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kuanika wizi na ubadhirifu wa fedha za umma, ingawa kazi yake hiyo imekuwa ikikwazwa na mamlaka husika kutotekeleza mapendekezo yaliyomo katika ripoti zake, ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha wote wahusika.
Hapa hatuwezi kusahau pia kuipongeza Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), kwani ripoti ya PAC imethibitisha kwamba tatizo la muda mrefu la upotevu wa fedha za Serikali kutokana na misamaha holela ya kodi limechochewa na wanasiasa kuingilia kazi za mamlaka hiyo.
Pengine yafaa tujiulize hapa kama ripoti ya PAC imeeleza ukweli, ukweli mtupu? Je, ni kweli kwamba fedha zilizowekwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuwa fedha za umma kama baadhi ya viongozi serikalini wamekuwa wakidai, licha ya vielelezo vilivyotolewa katika ripoti ya PAC?
Je, kuna watu watawajibishwa? Kuna viongozi watajiuzulu kutokana na ripoti hiyo kali iliyowasilishwa bungeni?
Tunauliza maswali hayo kutokana na kuwapo orodha ndefu ya watu wenye hadhi katika jamii ambao PAC imesema walilipwa fedha nyingi inayosemekana ilitoka katika akaunti hiyo ya Tegeta Escrow.
Kama itagundulika kwamba fedha walizolipwa zilikuwa za umma, kwamba zilipaswa kupelekwa Tanesco, waliolipwa fedha hizo watalazimishwa kuzirudisha? Maswali haya na mengine bila shaka yanaumiza vichwa vya Watanzania, hasa wakati huu ambao kuna mjadala mkali kuhusu jambo hilo ndani na nje ya Bunge.
PAC imetoa mapendekezo yake, hivyo mjadala wa mapendekezo hayo utakapomalizika, Bunge litajadili utetezi wa watu wote waliotuhumiwa katika ripoti hiyo na kufanya uamuzi. Wananchi wengi bila shaka watafuatilia maazimio ya Bunge kwa shauku kubwa.
Jambo la msingi hapa ni jinsi Serikali itakavyoipokea ripoti hiyo ya PAC na mapendekezo yake, hasa baada ya baadhi ya watendaji wake kupewa taswira hasi na kuonekana mbele ya jamii kama maadui wa taifa na wananchi, ambao wanapaswa kuwatumikia kwa uzalendo na moyo mkubwa? Hili ni jambo muhimu sana kwa Serikali, kwani mpira tayari umepigwa golini kwake.
Pamoja na kwamba jana bungeni Serikali ilipewa fursa ya kujibu hoja na tuhuma zilizoelekezwa kwake na ripoti ya PAC, ukweli ni kwamba hadhi na heshima yake ni kitu muhimu sasa pengine kuliko wakati wowote. Hadhi ya baadhi ya viongozi wa Serikali kwa namna moja ama nyingine imeguswa.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم