Na Fuad Ahmed, Mogadishu
Vikosi vya usalama vya Somalia vimekuwa vikifanya operesheni ya saa 24
huko Mogadishu tangia mwanzoni mwa mwezi wa Novemba, vikizuia
mashambulio yapatayo 20 na kukamata dazeni za viongozi wa al-Shabaab na
wapiganaji zaidi ya 20 wa al-Shabaab, kwa mujibu wa Wizara ya Usalama ya
Taifa.

Vikosi vya usalama vya Somalia na raia
wakiwa wamesimama karibu na eneo ambalo gari lililolipuliwa kwa bomu
katika barabara ya Maka al-Mukarama huko Mogadishu tarehe 16 Novemba,
2014. [Abdifitah Hashi Nor/AFP]
Al-Shabaab ilikuwa imepanga shambulio la kujitoa muhanga likilenga
wakaazi wa wilaya ya Dharkenley waliokuwa wakienda kwenye sala ya
alfajiri Ijumaa iliyopita (tarehe 14 Novemba), alisema msemaji wa wizara
Mohamed Yusuf Osman, lakini vikosi vya usalama viliweza kuzuia
shambulio hilo.
"Tuliwakamata watu watano ambao walikuwa wamejiandaa kutekeleza ulipuaji
wa bomu la kujitoa muhanga na mtu ambaye alikuwa amewapa hifadhi, [na
kunyang'anya] fulana nne za mlipuko ambazo zilikuwa kwenye mikoba ya
akina mama," aliiambia Sabahi.
"Wote walikuwa wanataka kulipua bomu la kujitoa muhanga dhidi ya umma
Ijumaa asubuhi, lakini tuliweza kuzuia hilo kutokana na taarifa
tulizopokea kutoka kwa raia wa wilaya ya Dharkenley huko Mogadishu,"
alisema.
Wakati wa operesheni hii, vikosi vya usalama vilikamata silaha na magari
matano ambayo al-Shabaab ilikuwa ikiyatumia kupiga risasi huku
wakiendesha, likiwemo gari lililotumiwa katika mauaji ya sababu za
kisiasa ya watunga sheria watano wa Somalia, akiwemo Saado Ali Warsame.
"Magari hayo pia yalitumiwa kufanya utoroshaji na uuaji wa raia kadhaa," Osman alisema.
"Serikali pia imechukua nyumba nne na gereji tatu ambazo zilikuwa zinatumiwa kama ngome ya kuandalia milipuko," alisema.
Osman aliwaomba wakaazi wa Mogadishu kuwa watulivu na kuwa na tahadhari
kuhusu mahali wanakoegesha magari yao ili wahusika wa al-Shabaab
wasiweke milipuko kwenye magari yao.
"Usalama kamili sio kitu ambacho kinaweza kufanikiwa [mara moja],"
alisema, akiuomba umma kutokata tamaa kwa mashambulio ya mara kwa mara
ya kikundi.
"Kinachotokea sasa ni kwamba al-Shabaab wanatapatapa kwa kukata tamaa
kwa kushindwa kufanikisha malengo yake baada ya kushindwa [na Somalia na
vikosi washirika]," Osman alisema. "Sasa, wanataka kuwaumiza raia na
kusababisha maangamizi ili waweze kusema, 'Bado tuko hapa na
tumesababisha mlipuko'."
"Lakini matatizo na uharibifu ambao umeletwa na al-Shabaab ni mkubwa
kuliko hilo, hivyo hebu tusizingatie kufedheheka na tuendelee kuunga
mkono mfumo wa usalama," alisema.
Hatua za ziada za usalama zinatakiwa
Kanali mstaafu wa jeshi la taifa la Somalia Dahir Timaadde alikaribisha
operesheni ya usalama ya hivi karibuni lakini alisema bado kuna dosari
za usalama ambazo zinahitaji kushughulikiwa.
"Vikosi vya usalama haviko katika hali inayofanana kama vilivyokuwa
miaka mitatu iliyopita wakati vilipokuwa na uhaba wa vifaa," aliiambia
Sabahi. "Hata hivyo, bado inaonekana kuna masuala mengi kutokana na
ukweli kwamba mauaji bado yanatokea kwenye makutano ya barabara kuu kwa
sababu hakuna vikosi vya usalama."
Serikali ya Somalia inapaswa kuweka magari ya polisi katika kila
makutano huko Mogadishu ili kushughulikia dharura kwa wakati, Timaadde
alisema.
"Tunaendelea kusikia kwamba makundi katika magari yamewaua watu
wanaofanya kazi na serikali na walifanikiwa kukimbia tukio hilo la
uhalifu," alisema. "Hilo linaonyesha kukosekana kwa uwezo wa vikosi vya
usalama. Serikali inatakiwa kuja na mpango kamili wa kuzuia majanga
hayo."
"Wakati ninajua kwamba usalama hauko thabiti kama ulivyopaswa kuwa,
vikosi vya usalama vinastahili sifa yetu kwa kuwa wameshiriki katika
jitihada za kuhakikisha usalama," alisema mkaazi wa Mogadishu mwenye
umri wa miaka 25 Maryam Mohamud, ambaye alisoma utawala wa umma katika
Chuo Kikuu cha Somalia.
"Tunapaswa kushirikiana nao kwa moyo wote ili kutokomeza ugaidi,"
aliiambia Sabahi, akitoa wito kwa raia kuongeza msaada wao kwa vikosi
vya usalama ili jiji liishi kwa amani.
Mohamud pia alitoa wito kwa serikali kuhamasisha wapiganaji wa
al-Shabaab kubadilika wenyewe chini ya programu ya msamaha na
kuwahakikishia usalama wao ili waamini jitihada hizo.
"Serikali inapaswa kuendesha kampeni ya uelimishaji inayoendelea ili
kuwafanya watu wanaotaka kubadilika wenyewe kujua kuwa hawatakabiliwa na
matatizo yoyote," alisema. "Serikali inapaswa pia kuongeza idadi ya
vituo vya mabadiliko ili wenye itikadi ya msimamo mkali wangebadilishwa
fikra [kuamini] wameacha kutoka katika mawazo yao."
Vijana pia wanapaswa kupewa mafunzo ya ufundi ili kwamba waweze kutafuta
kazi za kuwasaidia wao wenyewe na kutoamuliwa kujiunga na al-Shabaab
kwa kuahidiwa fedha, alisema Mohamud, akiwaomba washirika wa kimataifa
wa Somalia na mashirika ya msaada kuunga mkono jitihada hizo.
Chanzo: sabahionline.com
إرسال تعليق