
Hiyo haiakisi jitihada za serikali za Matokeo Makubwa Sasa (BRN), kwani hayo ni matokeo ya wastani tu wala si makubwa.
Tunajitahidi kuanzisha mipango na mikakati ya
kufufua elimu, tulikuwa na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi
(MMEM), Elimu ya Msingi kwa Wote (Universal Primary Education -UPE) na
mipango mingine mingi tu, lakini kimsingi haijasaidia kuinua kiwango cha
elimu nchini.
Watanzania tunajitahidi kuweka dawa ya kidonda
katika kidonda ambacho kimeota gaga (gamba), dawa zozote tutakazoziweka
juu ya gaga ni dhahiri kuwa hazitaponyesha kidonda kwa sababu kipo kitu
kinachozuia dawa isifike kwenye kidonda.
Ili kutatua tatizo hilo tunapaswa kuliondoa gaga
kwanza na gaga hili la elimu ni mfumo. Mfumo wetu wa elimu bado ni wa
mwaka 1947, si mfumo kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania, bado ni mfumo
wa kikoloni uliokuwa na dhamira ya kumwelimisha Mwafrika kusoma na
kuandika ili aweze kutekeleza kazi alizopangiwa kama vile ukarani,
upolisi na ualimu.
Miaka 53 sasa tokea tupate Uhuru, tumekuwa
tunauweka viraka tu mfumo wetu wa elimu badala ya kuufumua na kuunda
upya kutokana na mahitaji na matakwa yetu na matakwa ya maendeleo ya
karne tuliyonayo.
Bahati mbaya zaidi hata huo mfumo tulionao na
ambao tumeuzoea tunashindwa kuutendea haki kwa sababu ya kuwa na
miundombinu ya elimu iliyo dhaifu na hafifu.
Tunalifanya suala la elimu kama la kisiasa badala
ya kuwa la kitaaluma na kimkakati, tunapaswa tuweke vipaumbele vyetu
vyote katika elimu kama tunataka kuondokana na hali hii ya mkwamo wa
kimaendeleo tulionao.
Inashangaza kuona kwamba kila mwaka serikali yetu
inaainisha vipaumbele kati ya saba na nane katika bajeti ya Serikali.
Haya ni makosa makubwa kwani kwa kuwa tuna rasilimali chache, tukiwa na
vipaumbele vingi maana yake tumekusudia kugawana umaskini.
Zipo nchi ambazo katika miaka ya 60 uchumi wake
ulikuwa sawa na uchumi wa Tanzania, hivi leo zinashangaza dunia kwa
jinsi uchumi wake unavyopaa. Nchi kama Korea ya Kusini, Malaysia na
Singapore (kwa kuzitaja chache) ni nchi za kupigiwa mfano, zimeweka sera
na mikakati ya kuinua uchumi sio tu wa nchi bali hata wa wananchi wake
na silaha kubwa waliyoitumia ni elimu.
Kwanza walijivua kutokana na kamba za ukoloni,
waliondosha mfumo kandamizi wa elimu na kuweka mfumo huru kwa wananchi
wake na kufundisha kwa kutumia lugha wanayoielewa, lugha yao mama na
wala si Kiingereza, Kifaransa, Kiitaliano au Kireno.
Sisi huku kwetu uamuzi wa kutumia Kiswahili kama
lugha ya kufundishia umegeuzwa uamuzi wa kisiasa. Kwetu sisi bado
tumebaki na kasumba za kikoloni, usipojua Kiingereza hujasoma vyema na
hata fursa za kuajiriwa huwa chache. Bado tunakubali kubaki na
tongotongo za ukoloni.
إرسال تعليق