Wananchi Serengeti waikumbuka rasimu ya pili ya Jaji Warioba

Serengeti. Baadhi ya wananchi waliokuwa wanafuatilia mjadala wa escrow juzi, katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti, Mkoa wa Mkoa wa Mara walikumbuka Rasimu ya Pili ya Katiba iliyotupwa iliyokuwa ikitenganisha mihimili, hasa baada ya Spika Anna Makinda kuyumba kwa kuhofia mgongano wa mihimili na kusababisha kuvunjika kwa kikao cha Bunge.
Wananchi hao walioonekana kukerwa na jinsi mjadala mzima ulivyovurugika kutokana na kiti kuyumba, walisema kwamba rasimu ilikuwa inabainisha Spika na mawazili wasiwe wabunge ili kutenga misingi ya uwajibikaji.
Katibu wa CUF Wilaya ya Serengeti, Vedastus Makaranga alisema wananchi wanatakiwa kufuatilia mjadala kama huo ili kupima uzalendo wa wawakilishi wao, kwa kuwa matatizo mengi yanachangiwa na mfumo wa kutokuwajibika kwa viongozi wenye dhamana kwa misingi ya kulindana kivyama.Katika hatua nyingine, wananchi hao waliwataka wabunge wabunge kutoa uamuzi unaolenga kuleta heshima ya nchi, kwa waliohusika na upotevu wa mabilioni ya fedha kwenye sakata la escrow.
Sospeter Mabirika Mkazi wa mjini Mugumu alisema wabunge waache ushabiki wa vyama, kwenye suala ambalo madhara yake yameshaanza kuonekana kwa jamii, kutokana na nchi wahisani kusitisha uchangiaji wa bajeti ya maendeleo.
“Kila mbunge kabla ya uamuzi aangalie wapigakura kura wake wanavyokosa huduma mbalimbali na kama fedha zilizochotwa zingepatikana zingeweza kusaidia kutoa huduma, watu wanakimbia miji kwa kushindwa kuchangia maabara, huku wanaohujumu wanakingiwa kifua,” alisema.
“Haya yote yanahitaji busara ya hali ya juu katika kuyafanyia uamuzi kwani wananchi wamekuwa wakiishi maisha magumu na baadhi yao wakifaidika na rasilimali za nchi.’’

Post a Comment

أحدث أقدم