Waraka wa kuvuruga uchaguzi wafichuka

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinadaiwa kuandaa mkakati wa kuvifanyia hujuma vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili kuhakikisha havishindi uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na ule mkuu wa 2015.
Kwa mujibu wa waraka wa siri ambao umesambazwa wilayani Muleba mkoani Kagera bila kusainiwa, chama hicho kimeainisha malengo saba ya kufanyiwa kazi ili kudhibiti ushindi wa Ukawa.
Waraka huo ambao gazeti hili limeona nakala yake umepewa kichwa cha habari kisemacho ‘Maelekezo kwa viongozi wa CCM, Mbinu saba za mkakati wa kujumu wagombea wa Ukawa katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2014’.
Maelekezo ya mkakati huo uliogawanywa katika maeneo saba unaanza kwa kuwataka wana CCM kuandaa mgombea atakayetoka nje ya Ukawa lengo lilikwa ni kupunguza nguvu ya umoja huo.
Katika hilo, pia CCM wanadaiwa kuchonga mihuri ya vyama vya upinzani visivyokuwa na wafuasi kwenye maeneo ili waweze kuwachukuliwa fomu na kuwaweka kama wagombea kisha wajitoe baada ya mgombea wa Ukawa kuenguliwa kwa makosa mbalimbali.
Utekelezaji namba mbili ni kumteka nyara au kumlewesha mgombea anayetokana na Ukawa ili asiweze kurudisha fomu ya kuwania nafasi anayoiomba.
Lengo namba tatu ni wana CCM kufanya kila linalowezekana kumnunua mgombea anayetokana na Ukawa ili asirudishe fomu.
Namba nne katika mpango huo unaodaiwa na wachambuzi wa kisiasa kuwa ni ubakaji wa demokrasia, ni CCM kuhakikisha wanaweka mapingamizi kwa wapiga kura wa Ukawa wakati wa kujiandikisha na pia kumuwekea pingamizi mgombea yeyote asiyetokana na matakwa yao.
Pia katika mkakati huo unaodaiwa kuwahusisha wakurugenzi wa manispaa, halmashauri na miji, CCM wameazimia kuhakikisha wanaopata nafasi ya kuandikisha wapiga kura anakuwa ni kada wao na jukumu la watu hawa ni kuhakikisha kundi linalounga mkono Ukawa halipewi nafasi ya kujiandikisha.
Katika kipengele hicho, wale watakaopata nafasi ya uandikishaji watatakiwa kuomba udhuru wa kuahirisha uandikishaji kwa muda atakaoona kundi kubwa la vijana likitaka kujiandikisha.
Hujuma ya sita ni kuwahimiza wafuasi wa CCM kuanzisha fujo wakati wa kuhesabu kura ili kura zikahesabiwe katika eneo la majumuisho na lengo ni kutoa nafasi ya kuweza kubadilisha masanduku ya kura wakati yanapopelekwa katika eneo la majumuisho.
Saba katika waraka huo usioonesha moja kwa moja ushiriki wa viongozi wa kiserikali, unatoa maagizo kwa mamlaka hizo kuhakikisha matendo yote yanayoiondolea CCM imani kwa wananchi yanasimamishwa mpaka mwaka 2016.
Mambo yanayotakiwa kusimamishwa katika mkakati huo ni pamoja na kusitisha suala zima la bomoa bomoa ya vibanda vya wafanyabiashara, kutowabughudhi madereva wa boda boda, kuwaacha Mama na Baba Ntilie wafanye shughuli zao kwa uhuru na kwamba agizo hilo lianze mapema.
Diwani wa Kata ya Muleba, Hassan Milanga (CUF), alipoulizwa kuhusu uwepo wa waraka huo, alisema amepata taarifa ingawa bado hajauona, huku akilaani kitendo hicho kuwa ni hofu ya watawala kuondolewa katika nafasi zao.
Katibu wa CCM Wilaya ya Muleba, Anatory Nshange, alikanusha chama chake kuhusika na waraka huo huku akieleza kama kuna watu wanaochonga mihuri ya vyama vingine pasipo ridhaa ya chama husika kuwa wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema CCM haiwezi kufanya jambo hilo la kuandaa waraka kwa kile alichoeleza chama chake kimejiandaa vya kutosha kushinda katika uchaguzi.
“Habari hizi ni uzushi, juzi tulikutana viongozi wa vyama mbali mbali pamoja na wahusika wa uchaguzi na tukakubaliana namna ya kufanya uchaguzi kistaarabu kama kulikuwa na suala hilo si wangesema hapo hapo,”alisema Nshange.
- Tanzania Daima

Post a Comment

Previous Post Next Post