CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinadaiwa kuandaa mkakati wa kuvifanyia
hujuma vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili
kuhakikisha havishindi uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na ule mkuu
wa 2015.
Kwa mujibu wa waraka wa siri ambao umesambazwa wilayani Muleba mkoani
Kagera bila kusainiwa, chama hicho kimeainisha malengo saba ya
kufanyiwa kazi ili kudhibiti ushindi wa Ukawa.
Waraka huo ambao gazeti hili limeona nakala yake umepewa kichwa cha
habari kisemacho ‘Maelekezo kwa viongozi wa CCM, Mbinu saba za mkakati
wa kujumu wagombea wa Ukawa katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2014’.
Maelekezo ya mkakati huo uliogawanywa katika maeneo saba unaanza kwa
kuwataka wana CCM kuandaa mgombea atakayetoka nje ya Ukawa lengo
lilikwa ni kupunguza nguvu ya umoja huo.
Katika hilo, pia CCM wanadaiwa kuchonga mihuri ya vyama vya upinzani
visivyokuwa na wafuasi kwenye maeneo ili waweze kuwachukuliwa fomu na
kuwaweka kama wagombea kisha wajitoe baada ya mgombea wa Ukawa
kuenguliwa kwa makosa mbalimbali.
Utekelezaji namba mbili ni kumteka nyara au kumlewesha mgombea
anayetokana na Ukawa ili asiweze kurudisha fomu ya kuwania nafasi
anayoiomba.
Lengo namba tatu ni wana CCM kufanya kila linalowezekana kumnunua mgombea anayetokana na Ukawa ili asirudishe fomu.
Namba nne katika mpango huo unaodaiwa na wachambuzi wa kisiasa kuwa
ni ubakaji wa demokrasia, ni CCM kuhakikisha wanaweka mapingamizi kwa
wapiga kura wa Ukawa wakati wa kujiandikisha na pia kumuwekea pingamizi
mgombea yeyote asiyetokana na matakwa yao.
Pia katika mkakati huo unaodaiwa kuwahusisha wakurugenzi wa manispaa,
halmashauri na miji, CCM wameazimia kuhakikisha wanaopata nafasi ya
kuandikisha wapiga kura anakuwa ni kada wao na jukumu la watu hawa ni
kuhakikisha kundi linalounga mkono Ukawa halipewi nafasi ya
kujiandikisha.
Katika kipengele hicho, wale watakaopata nafasi ya uandikishaji
watatakiwa kuomba udhuru wa kuahirisha uandikishaji kwa muda atakaoona
kundi kubwa la vijana likitaka kujiandikisha.
Hujuma ya sita ni kuwahimiza wafuasi wa CCM kuanzisha fujo wakati wa
kuhesabu kura ili kura zikahesabiwe katika eneo la majumuisho na lengo
ni kutoa nafasi ya kuweza kubadilisha masanduku ya kura wakati
yanapopelekwa katika eneo la majumuisho.
Saba katika waraka huo usioonesha moja kwa moja ushiriki wa viongozi
wa kiserikali, unatoa maagizo kwa mamlaka hizo kuhakikisha matendo yote
yanayoiondolea CCM imani kwa wananchi yanasimamishwa mpaka mwaka 2016.
Mambo yanayotakiwa kusimamishwa katika mkakati huo ni pamoja na
kusitisha suala zima la bomoa bomoa ya vibanda vya wafanyabiashara,
kutowabughudhi madereva wa boda boda, kuwaacha Mama na Baba Ntilie
wafanye shughuli zao kwa uhuru na kwamba agizo hilo lianze mapema.
Diwani wa Kata ya Muleba, Hassan Milanga (CUF), alipoulizwa kuhusu
uwepo wa waraka huo, alisema amepata taarifa ingawa bado hajauona, huku
akilaani kitendo hicho kuwa ni hofu ya watawala kuondolewa katika
nafasi zao.
Katibu wa CCM Wilaya ya Muleba, Anatory Nshange, alikanusha chama
chake kuhusika na waraka huo huku akieleza kama kuna watu wanaochonga
mihuri ya vyama vingine pasipo ridhaa ya chama husika kuwa wanapaswa
kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema CCM haiwezi kufanya jambo hilo la kuandaa waraka kwa kile
alichoeleza chama chake kimejiandaa vya kutosha kushinda katika
uchaguzi.
“Habari hizi ni uzushi, juzi tulikutana viongozi wa vyama mbali mbali
pamoja na wahusika wa uchaguzi na tukakubaliana namna ya kufanya
uchaguzi kistaarabu kama kulikuwa na suala hilo si wangesema hapo
hapo,”alisema Nshange.
- Tanzania Daima
إرسال تعليق