Warioba aitaabisha serikali

    Mbunge wa Rombo Joseph Selasini
  • Mbunge afichua pia jinsi familia ya Nyerere inavyodhalilishwa
MZIMU wa kumshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji mstaafu, Joseph Warioba umeibukia tena bungeni baada ya Mbunge wa Rombo Joseph Selasini (CHADEMA) kuhoji kwanini ameondolewa walinzi na Serikali.
Katika swali hilo, mbunge huyo alitaka Serikali ieleze ina mkakati gani wa kuimalisha ulinzi kwa wastaafu waliokuwa viongozi wakuu wa taifa, akiwamo Jaji Warioba ambaye amepata kuwa Waziri Mkuu.
Selasini aliihoji serikali ina mikakati gani ya kuwalinda wazee hao mbao walikuwa walilitumikia taifa, lakini baadhi yao hivi sasa wanatishiwa maisha na kudhalilishwa.
“Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tumeona jinsi mzee wetu, Jaji Joseph Warioba alivyodhalilishwa kwa kutaka kupigwa na vijana wa kihuni jijini Dar es Salaam kwanini hana ulinzi au ndio ameondolewa ulinzi? alihoji Selasini.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani alisema viongozi wote wastaafu wanalindwa na wanatunzwa na serikali.
Alisema serikali ina viongozi wastaafu 13 ambao wamewahi kuwa marais na mawaziri wakuu na kwamba wote wana walinzi na wanatunzwa na serikali kwa mujibu wa sheria.
“Mfano ni hapa bungeni, si unamwona Mheshimiwa Lowassa ana walinzi wawili na hao wengine, wote wana walinzi na wanatunzwa vizuri na serikali, hata Jaji Warioba anao walinzi labda kama aliwaacha siku hiyo,” alisema Kombani.
Majibu hayo, yalimwinua tena Seleasini na kuomba mwongozo wa Spika kuonyesha kutoridhishwa na majibu mepesi ya Waziri Kombani.
Selasini alisema Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi aliwahi kupigwa kofi hadharani, Rais Kikwete alishawahi kuvamiwa jukwaani kule Mwanza na kwamba juzi Watanzania  wameona jinsi Jaji Warioba alivyofanyiwa.
“Ukiacha mbali wazee hao kushambuliwa, Mama Maria Nyerere alishawahi kulalamika hana maji, kule Butiama nyumbani kwa baba wa Taifa hakuna maji, chooni unaingia na ndoo na kopo, pia Msasani maji yamekatwa, hata jenereta lililopo ni bovu la mwaka sabini, lakini Waziri anakuja na majibu mepesi.
“Kama hilo Jina la Warioba linawauma wengine vifuani mwenu hamtaki kulisikia basi vumilieni lakini suala la msingi hapa ni usalama wa maisha ya viongozi wetu wastaafu wala hakulengwa mmoja kama waziri alivyojibu hapa,” Mheshimiwa Naibu Spika naomba mwongozo wako.
Awali katika swali la msingi la Selasini alitaka kujua serikali ina wazee wangapi wa kuanzia miaka sitini na kuendelea na kama kuna mkakati wa kuwapa huduma mbalimbali kama vile chakula, malazi, matibabu na kadharika.
Aidha alitaka kujua kama serikali haioni umuhimu wa kuanzisha kitengo maalum cha kuwatambua, kuwahudumia na kuwaenzi kama ilivyo kwa watoto na akina mama.
- Tanzania Daima

Post a Comment

أحدث أقدم