Watu 16 kizimbani wakidaiwa kuharibu mali za mwekezaji

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama.
Watu 16 wamefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kujibu mashtaka ya kuvamia, kuharibu na kuchoma moto mali zenye thamani ya shilingi bilioni 1.7 za mwekezaji, Peter Jones, raia wa Uingereza.
 Katika washtakiwa hao waliofikishwa mahakamani hapo jana,  wamo wafugaji 13 wa jamii ya Wamasai kutoka wilaya ya Longido mkoani Arusha na Siha ya Kilimanjaro.

Mwendesha Mashtaka, Inspekta wa Polisi,   Roymax Membe, mbele ya ya Hakimu Mfawidhi, Denis Mpelembwa aliwataja washtakiwa hao kuwa ni   Matey Hilita (42), Julius Daudi (45), Elipokea Sefano (42), Andrea Elias (67), Alex Philipo (30), Victor Joakimu (32), Dickson Mallya (38), ambao ni wakazi wa kijiji cha Miti Mirefu.

Wengine ni  Dickson Kweka (62), Emanuel Isaya (17), ambao ni wakazi wa Sanya Juu; Erick Wilson (27), Rahel Paulo (26), Bibiana Charles (36), Hellen Stepahano (39), Hellen Daudi (26) na Monica Rongai (42), wakazi wa wa kijiji cha Miti Mirefu.

Inspekta Membe, alidai kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Novemba 14, mwaka huu baada ya kuvamia shamba la Ndarakwai linalomikiwa na mwekezaji huyo.

Alidai kuwa katika shtaka la kwanza washtakiwa hao wanadaiwa kuwa waliingia ndani ya shamba la Ndarakwai na kuchoma magari 11 ya kambi ya utalii ya Ndarakwai yenye thamani ya Sh.  milioni 450 kinyume na kifungu cha 299 cha sheria ya mwenendo wa  makosa ya jinai cha mwaka 2002.

Mwendesha mashtaka huyo alidai  katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa  kuharibu mali za mwekezaji huyo kwa makusudi, zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni moja na la tatu ni kuchoma mali zake  zenye thamani ya Sh. milioni 210  kinyume cha kifungu cha 326 (i) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002

Hata hivyo, alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo kuwanyima dhamana washtakiwa hao kwa kuwa thamani halisi ya vitu vilivyoharibiwa haijafahamika.

Hakimu Mpelembwa alikubali ombi hilo na  kutoa siku saba awakilishe thamani halisi ya uharibifu huo. Washtakiwa hao walikana mashtaka na kesi hiyo kuahirishwa hadi Desemba 2, mwaka huu itakapotajwa tena.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post