
KATI ya watu 4,879 mkoani hapa waliopima afya zao kwa hiari katika
kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septembam waka huu, 305
wamebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).
Akizungumza katika kikao cha utekelezaji wa shughuli za Ukimwi
zilizotekelezwa na Kamati ya Kudhibiti Ukimwi mbele ya Baraza la
Madiwani juzi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Meya wa
Manispaa ya Iringa, Gervas Ndaki, alisema kati ya waliojitokeza kupima
na kupata ushauri nasaha, wanaume walikuwa 2,417 na wanawake 2,467.
Ndaki, alisema kati ya watu 305 waliopima kwa hiari na kukutwa na maambukizi, wanaume walikuwa 124 na wanawake 181.
Alisema huduma ya kuzuia maambukizi ya vvu/ukimwi kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto, wajawazito 1,036 walijitokeza na kupata ushauri
nasaha na kupima, kati yao wajawazito 10 sawa na asilimia moja walikutwa
na maambukizi.
Ndaki, alisema mapambano ya ukimwi yanaambatana na huduma za tiba sahihi ya magonjwa ya ngono.
Alisema kuwa moja ya njia ya kupambana na maambukizi mapya ni tohara
kwa wanaume na waliojitokeza walikuwa 539 ambao walitahiriwa na kati ya
hao waliokutwa na maambukizi ya vvu walikuwa saba.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa,
Amani Mwamwindi, aliwataka watendaji kuweka mkazo katika mapambano
dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, kwa kuwasisitiza
wananchi kwa kuwapa elimu kuondokana na maambukizi mapya.
- Tanzania Daima
إرسال تعليق