
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
*
Mwekezaji wa Poland asema wataanza kujenga Januari, mwakani
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amekagua maghala ya
kuhifadhia chakula yaliyopo Kizota nje kidogo ya mji wa Dodoma ikiwa ni
utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Alhamisi iliyopita kwamba Serikali inalenga
kujenga maghala kwenye mikoa sita kupitia mkopo ambao itaupata kutoka Serikali
ya Poland.
Akizungumza
na viongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA) leo asubuhi (Alhamisi, Novemba 6, 2014) wakati akikagua maghala hayo,
Waziri Mkuu alisema katika mkoa huo, Serikali ina nia ya kujenga maghala
makubwa (SILOS) yenye uwezo wa kuhifadhi tani 100,000 za nafaka kwa wakati
mmoja.
“Tukipata
maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 100,000 tutakuwa na uhakika wa kuchukua
na akiba ya nafaka kutoka mikoa ya jirani ya Singida, Tabora na Manyara,”
alisema.
Waziri
Mkuu alifuatana na Bw. WITOLD KARCZEWSKI ambaye ni
mmiliki wa kiwanda kikubwa cha kusindika nafaka
nchini Poland ambacho Waziri Mkuu Pinda alikitembelea alipozuru nchi hiyo
Oktoba 24, mwaka huu. Bw. KARCZEWSKI anamiliki pia kiwanda kinachotengeneza
malighafi za kujengea SILOS.
Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa kituo cha NFRA Kanda
ya Kati, Bw. Ruwaichi Mambali alisema kituo hicho kina maghala yenye uwezo wa
kuhifadhi tani 30,000 lakini kwa sasa kina tani 69,000 ambazo kati ya hizo tani
62,000 zipo Kizota (Dodoma) na tani 7,000 ziko Manyoni (Singida).
Alisema eneo zima la Kizota lina ukubwa ekari 33 na kwamba kuna
maghala matatu yenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 kila moja. “Lakini kwa sasa
tumelazimika kuweka mahindi mengine na mtama hapa nje ambayo tumeyafunika kwa
maturubali,” alisema.
Kwa upande wake, Bw. KARCZEWSKI alitaka kufahamu miundombinu
iliyopo kwenye ghala la Kiszota ikiwemo umabli wa kutoka barabara kuu pamoja na
reli. Pia alitaka kujua eneo zima lina ukubwa kiasi gani. Na alitaka kufahamu
mbinu zinazotumika hivi sasa kuhifadhi chakula kwenye ghala hilo.
Alisema wakipata michoro ya eneo hilo (site map), atatuma
wataalamu wake Januari mwakani waangalie uwezekano wa kuanza ujenzi mapema
iwezekanavyo pindi mazungumzo yakikamilika.
Alhamisi
iliyopita, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara
baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwl. Julius Nyerere akitokea Oman,
Waziri Mkuu alisema alikwenda Poland kutafuta msaada
wa mfumo wa mkopo wenye masharti nafuu ambao utasaidia kupambana na tatizo la
uhaba wa maghala kwa ajili ya kuhifadhia nafaka.
Alisema Serikali imelenga mikoa sita ya kuanzia ambayo ni Ruvuma,
Rukwa, Njombe (pamoja na Iringa) ambako kuna uzalishaji mkubwa wa mahindi. Pia
inaangalia Kanda ya Ziwa ambako mara nyingi wana uhaba wa chakula; na kwamba itaweka
maghala mkoani Dodoma kwa sababu ni katikati ya nchi ili ikusanye akiba kutoka
mikoa ya jirani ya Singida, Manyara na Tabora.
“Lengo
ni kupata uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 hadi 1,000,000 na ujenzi wao siyo
kama huu wa kwetu. Tumewaomba watujengee SILOS (maghala makubwa) kwa sababu
zina teknolojia ya kujua kiasi gani cha nafaka kimeingia, zina unyevu kiasi
gani, unaweza kuweka dawa nafaka zako, kuosha na kukausha na kisha ukasindika
kwa kiwango unachotaka,” Waziri Mkuu aliwaeleza waandishi wa habari.
Alisema uzalishaji mwaka huu umetoa ziada ya tani
milioni 1.5 za nafaka na tani 800,000 za mpunga ikilinganishwa na ziada ya tani
300,000 iliyokuwepo mwaka jana. “Serikali inakabiliwa na changamoto ya kupata
soko la uhakika kwa mazao ya wakulima kwa sababu tulizoea kumtumia Wakala wa
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kama mnununzi mkuu na uwezo wezo wake ni
tani 240,000 tu kwa mwaka,” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA
WA MAGOGONI,
11410 – DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, NOVEMBA 6, 2014
إرسال تعليق