Wiki ya Werema, Muhongo, Maswi

  • CCM wataka wang’oke kukinusuru chama
  • CHADEMA, CUF wamtaka JK asiwakingie kifua
Muhongo, Maswi, Werema, MACHO na masikio wiki hii yataelekezwa zaidi mjini Dodoma, kujua hatma ya watuhumiwa wanaodaiwa kuchota zaidi ya sh bilioni 300, zilizohifadhiwa kwenye Akaunti Maalum ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Wiki hii, Bunge linatarajia kutumia siku mbili kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyochunguza kashfa hiyo.
Habari kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM mjini hapa, zilibainisha kuwa wabunge wengi wameridhia watuhumiwa katika kashfa hiyo wawajibike kwa kuachia nafasi zao na kuhakikisha wanarejesha fedha hizo za umma.
Watuhumiwa katika kashfa hiyo waliotajwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ni pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambao wiki itakuwa chungu sana kwao.
Wengine ni Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba, huku Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitajwa kuhusika kutokana na uzembe wa watendaji wake kushindwa kusimamia rasilimali za taifa.
CHADEMA: JK usimbebe Pinda
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutomkingia kifua Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika sakata la kuchota fedha kwenye Akaunti ya Escow, zilizohofadhiwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, John Mnyika wakati akifungua mkutano wa siku mbili kwa mkatibu na viongozi mbalimbali wa mikoa wa Baraza la Vijana wa CHADEMA, (BAVICHA).
Alisema CHADEMA imenasa taarifa kwamba Rais Kikwete anashinikiza kutowajibishwa kwa Waziri Mkuu kuhofia Serikali yake kuanguka na ndio ameendelea kufumbia macho na kukaa kimya juu ya kashfa hiyo.
Mbali na Pinda, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, pia alimtaka Rais Kikwete kutokingia kifua watuhumiwa wengine katika kashfa hiyo kama watalazimika kuwajibika.
Alisema kashfa hiyo imetokana na udhaifu wa Rais Kikwete na Serikali, ambao umeisababishia taifa hasara kwa baadhi ya watu wachache kuchota fedha hizo bila kuchukuliwa hatua yoyote.
Huku akishangiliwa na makada wa CHADEMA, Mnyika alisisitiza hakuna sababu hata chembe ya kumkingia kifua Waziri Mkuu Pinda, Werema, Maswi na wengine, kwani kiasi cha fedha kilichochotwa ni kikubwa na kingeweza kusaidia hata ujenzi wa maabara kwa nchi nzima badala ya kuwachangisha wananchi sasa.
Akizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mnyika aliwataka viongozi hao wa vijana kuhakikisha wanajipanga kukabiliana na hujuma zinazofanywa na Serikali kwa ajili ya kuhujumu uchaguzi huo pamoja na uchaguzi mkuu ujao.
Alisema kuwa, hivi sasa kuna hujuma za baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani wanafanyiwa urasimu wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uchaguzi ili waonekane wameshindwa kufuata sheria.
Naibu Katibu Mkuu huyo, pia alilaani kauli za Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye, kwamba CHADEMA imesambaza waraka wa kutaka wagombea wote wawe wa CHADEMA badala ya Ukawa, jambo ambalo sio sahihi.
Alisema makubaliano ya Ukawa ni kusimamisha mgombea mmoja mwenye nguvu kwenye kila nafasi ya uchaguzi hadi urais ili kuing’oa CCM.
Mnyika, aliwataka vijana hao kufanya kampeni ya kuikataa Katiba pendekezwa kwani ikipitishwa ni sawa na kurejesha ufisadi zaidi nchini.
Jijini Dar es Salaam, Chama cha Wananchi (CUF), kimewataka Waziri Mkuu Pinda, Mwanasheria Mkuu Jaji Werema, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Muhongo pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Maswi, wajiuzulu au kufukuzwa mara moja.
Pia kimeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), iwachunguze haraka kama wamehusika na rushwa katika kuwezesha kampuni ya Pan African Power (PAP), ambayo imeshirikiana na viongozi wa serikali kuitapeli na kuibia fedha serikali kwa kuzichukua kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema viongozi hao moja kwa moja wanahusika katika kashfa hiyo, kwa kuwa hata Benki Kuu ilikuwa na wasiwasi kuwa fedha za Tegeta Escrow zilikuwa zinachukuliwa kinyume na utaratibu, lakini wao waliruhusu na kukaa kimya.
Alisema Mwanasheria Mkuu, alivunja sheria kwa kuelekeza kuwa kodi ya ongezeko la thamani kwenye tozo la uwekezaji ‘capacity charges’ isilipwe na kusababisha serikali kupoteza mapato ya sh bilioni 21.
Aliongeza kuwa, Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, hawakufanya uhakiki kuhusu uhalali wa umiliki wa kampuni ya IPTL na kusaini kutoa fedha za Escrow bila ya kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi, hivyo kulipotezea shirika zaidi ya sh bilioni 321.
Pia, alisema Mkurugenzi wa Shirika la Umeme (Tanesco), na Bodi ya shirika hilo, hawakutimiza wajibu wao wa kulinda maslahi ya shirika wanaloliongoza na kugeuza maamuzi yake yenyewe na kulikosesha sh bilioni 321, hivyo nao wanatakiwa kuachie ngazi.
Alisema Waziri Mkuu ambaye ndiye kiongozi wa Serikali bungeni na Msemaji Mkuu, alilipotosha Bunge, aliposema bungeni mwezi Mei kuwa fedha hizo sio za umma isipokuwa kodi.
Prof. Lipumba, alisema BoT iliwahi kuandika barua kwa viongozi hao ili kujiridhisha pia anaamini hata Rais Kikwete analifahamu suala hilo na aliamua kukaa kimya bila kuchukua hatua zozote.
“Hivyo tunamtaka Rais Kikwete aueleze umma kwa nini serikali yake ilishindwa kuzuia fedha za Tegeta Escrow zisiporwe wakati Benki Kuu ilionyesha wazi wasiwasi wake kuhusu uhalali wa kuhamisha fedha hizo,” alisema Prof. Lipumba.
Aidha, alisema sakata la Tegeta Escrow linaonyesha umuhimu wa Bunge kuisimamia Serikali na Wabunge kutokuwa mawaziri kama ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba na Tume ya Jaji Warioba kabla ya kuondolewa kwenye katiba inayopendekezwa.
Aliiongeza kuwa, baada ya ripoti ya CAG kukamilika, Waziri Mkuu amekuwa akitafuta visingizio vingi ili ripoti hiyo isijadiliwe bungeni .
Lipumba, alisema kuwa taarifa za vigogo wengi kupewa fedha kutoka akaunti inayomilikuwa na James Rugemalira inaonesha umuhimu wa kifungu kilichopendekeza zawadi za viongozi zirejeshwe serikalini, ambacho kimechakachuliwa ili kuruhusu viongozi wa serikali kuendelea kujichotea mali za Watanzania kwa njia ya hongo za zawadi

Post a Comment

أحدث أقدم