MBUNGE wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), amesema kuwa kati
ya Wizara ambazo zinalalamikiwa kwa uzembe ni Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi.
Khalifa, aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la
nyongeza kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
George Simbachawene.
Mbunge huyo, alisema kuwa Wizara hiyo imekuwa ikilalamikiwa na
Wananchi kwa uzembe kutokana na utendaji usioridhisha, jambo ambalo si
jema.
Aidha, Mbunge huyo alitaka kujua kama Wizara hiyo imekuwa ikiwakagua
Watumishi wake kwa kuangalia utendaji wao wa kazi na kama wamebaini
mapungufu, je wanatoa taarifa kwa Rais ili waweze kuchukuliwa hatua
stahiki?
Pia, alitaka kujua hadi sasa kuna Wafanyakazi wangapi wa Wizara ya
Ardhi ambao wamefukuzwa kazi kutokana na utendaji mbovu wa kazi.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri George Simbachawene alisema kuwa
sekta ya Ardhi ni pana na imekuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa,
lakini pia ina Sheria zake.
Alisema kuwa, kutokana na upana huo wa sekta ya ardhi sheria zake
zimekuwa na migongano mingi licha ya kuwepo kwa juhudi katika
kuzitatua.
“Kila kukicha tumekuwa tukichukua hatua ambapo kila baada ya miezi
mitatu, tumekuwa tukimsimamisha mfanyakazi mmoja wa Wizara ya Ardhi
kutokana na makosa mbalimbali,” alisema.
Katika swali la msingi ambalo liliulizwa na Mbunge wa Tanga Mjini,
Omar Nundu (CCM), aliyetaka kujua je ni lini Serikali itatengua umiliki
wa mashamba ya mkonge ya Mkoa wa Tanga ili wananchi hao waishi maisha
ya amani.
Pia, alihoji Serikali inachukua hatua gani kuzuia tabia ya wamiliki
wa mashamba hayo kuuza kwa watu wengine endapo yatagunulika kama
yametekelezwa.
Akijibu maswali hayo, Simbachawene alisema kuwa Wizara yake
ilishawasilisha mapendekezo kwa Rais Jakaya Kikwete, kubatilisha miliki
za mashamba kwa Mkoa wa Tanga ambayo yametelekezwa kwa muda mrefu ili
zibatilishe.
“Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu Mheshimiwa Spika kuwa,
Mheshimiwa Rais ameridhia miliki za mashamba ya Bombwera, Kihuhwi,
Sagulas, Lewa, Kwafungo na Geigliyz/Kilapuka zibatilishwe ili haimaye
yagawiwe kwa wananchi,” alisema Naibu Waziri huyo.
Post a Comment